Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini ambapo ongezeko hilo limechangiwa na kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa hizo.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Februari 20,2023 Jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba 2023.
“Takwimu kutoka kwenye vituo vya MAT zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915 katika kuongeza ufanisi wa Mamlaka, Serikali imeanzisha kituo cha huduma kwa wateja (call centre) ili kutoa nafasi kwa wananchi kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya,” amesema Mhagama.
Aidha mesema kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata kilo 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini huku watuhumiwa wakiwa 10,522 ambapo kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821.
“Jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa, kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Pia Waziri Mhagama ameongeza kuwa Tanzania imekuwa kishirikiana na nchi mbalimbali za kikanda na kimataifa katika kupambana na dawa za kulevya ambapo ushirikiano huo unahusisha kubadilishana taarifa za kiusalama kuhusu dawa kulevya, na kujengeana uwezo katika mapambano hayo.
“Hivi karibuni tumesaini hati ya makubaliano kati ya Tanzania na Zambia kushirikiana kudhibiti biashara ya dawa za kulevya. Baadhi ya faida zilizotokana na ushirikiano huu ni kufanikisha ukamataji wa baadhi ya watuhumiwa wanaohusishwa na kilo 3,522. 52 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine zilizokamatwa mwezi Disemba, 2023 pamoja na ukamataji wa kilo 423.54 za skanka litokana na ushirikiano mzuri kati yetu na Zambia,”ameongeza Mhagama.