Uncategorized

WAHARIRI WAKUMBUSHWA MAADILI, KUWALINDA WATOTO MITANDAONI

Written by mzalendoeditor

 

Na WMJJWM, Dar Es Salaam

Serikali imewaomba Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kutumia nafasi zao kuwahimiza Wazazi na Walezi kuhakikisha wanafuatilia kwa usahihi matumizi ya vifaa vya kielektroniki ili watoto kuwa salama mtandaoni.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima jijini Dar Es Salaam Februari 09, 2024 alipozungumza na baadhi ya Wahariri waliopata mafunzo kuhusu usalama wa watoto mtandaoni kuelekea uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya kutokomeza ukatili wa watoto mtandaoni.

Waziri Dkt. Gwajima amewahimiza wahariri kutumia vyombo vyao kuwaelimisha Wazazi na Walezi kutimiza wajibu wao ikiwemo kuweka kiwango cha muda wa matumizi ya vifaa vya kieletroniki, kuhakikisha watoto wanatumia vifaa vya kielektroniki chini ya uangalizi wa karibu na
kuwaelimisha watoto wenyewe matumizi sahihi ya vifaa vya kieletroniki ili wasifanyiwe ukatili kupitia mitandao.

“Ni Imani yangu kuwa, semina hii itawajengewa uwezo na kuwaongezea ari ya kutoa mchango wenu katika kuhakikisha usalama wa mtoto mtandaoni unaeleweka kwa jamii.” Amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba, kutokana na kukua kwa teknolojia ya Habari na mawasiliano ni dhahiri matumizi ya vifaa vya kielektroniki hasa kwa watoto ni haikwepeki japo kuna changamoto ya kuelewa na kufahamu fursa na hatari ambazo intaneti inaweza kuleta.

“Kutokana na hilo vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika kuelimisha watoto, wazazi/walezi na jamii kwa ujumla kuhusu faida na changamoto za usalama wa watoto mtandaoni” ameongeza Waziri Dkt. Gwajima.

Amebainisha pia pamoja na faida nyingi za mitandao, athari zinazowakuta watoto katika matumizi ya mitandao bila uangalizi wa karibu zinajumuisha kuanza ngono katika umri mdogo, athari za kisaikolojia na mmonyoko wa maadili unaotokana na mwingiliano wa mila na desturi za mataifa mengine ikiwa pamoja na ushoga na usagaji.

Kampeni hiyo ya Kitaifa itakayokuwa na kaulimbiu ya “Usalama wa Mtoto Mtandaoni ni Jukumu Letu; Chukua Hatua” inatokana na jitihada za Serikali na wadau za kutoa elimu ya usalama wa watoto mtandaoni na itazinduliwa Februari 10, 2024 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor