Kitaifa

MCHENGERWA:ALAT SIMAMIENI NIDHAMU YA MADIWANI NA WAKURUGENZI

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kushuka kwa nidhamu ya baadhi ya madiwani na wakurugenzi ni matokeo ya kulegalega kwa utendaji kazi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).

Waziri Mchengerwa amesema jukumu la msingi la (ALAT) ni kuimarisha nidhamu na ushirikiano baina ya baraza la madiwani na watendaji wa serikali kuhakikisha wanaongea lugha moja katika kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Amesema “Msingi wa uanzishwaji wa (ALAT) mwaka 1984, baba wa taifa Julius Kambarage Nyerere alikusudia mengi ambayo kama (ALAT) wakifanya vizuri leo, wataweza kutusaidia kuyaboresha na kutuweka sawa”

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo katika kikao kazi kilicho wakutanisha wajumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na viongozi wa juu wa OR – TAMISEMI na PPRA kilicholenga kujadiliana namna bora ya kuboresha utendaji kazi wa jumuiya hiyo.

Akizungumzia madai ya uwepo wa baadhi ya mifumo inayokwamisha manunuzi, Waziri Mchengerwa amesema wakati mwingine viongozi wa ngazi za juu wamekuwa wakichukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hasa wakurugenzi kwa madai ya kuchelewesha manunuzi ilihali wakati mwingine wakurugenzi wakikwamishwa na mifumo.

“Tumejikuta tunalazimika kuwaadhibu wakurugenzi, kumbe wakati mwingine makosa siyo yao ni ya mifumo ya manunuzi au pengine ni mipya kwao ama hawana elimu au uelewa wa kutosha kuhusiana na mifumo hiyo” alisema Waziri Mchengerwa

Ili kupata utatuzi wa hoja hizo za kimsingi zinazodaiwa kukwamisha utendaji kazi wa baadhi ya halmashauri, waziri Mchengerwa alimpa fursa afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA Bw. Eliakim Maswi kutoa ufafanuzi wa kina na elimu juu ya namna mifumo ya manunuzi inayotumiwa na serikali inavyopaswa kufanya kazi.

Akiongea kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo mwenyekiti wa ALAT Taifa Mhe. Murshid Ngeze, amepongeza hatua ya kukutanishwa na watendaji wa juu wa OR – TAMISEMI na PPRA na kusema kuwa wamefarijika kukutanishwa na viongozi hao na kikao hicho ni mwanzo wa kwenda kuonesha uimara wa serikali za mitaa na kuondoa kero ndogondogo ambazo zinamchukiza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu.

About the author

mzalendo