Featured Kitaifa

MAHUNDI ASHIRIKI MKUTANO WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI BONDE LA ZIWA VICTORIA KENYA.

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) leo Februari 9, 2024 ameshiriki kwenye Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria, Jijini Kisumu nchini Kenya akimuwakilisha Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso(Mb).

Mkutano huo, umepitia taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na taarifa ya Kamati za kikanda za Makatibu Wakuu, za uendeshaiji wa programu na miradi ya kamisheni ya bonde hilo.

Aidha agenda za Mkutano huo ziligawanyika katika makundi mawili ya Utekelezaji wa Miradi, pamoja na Utafutaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Miradi inayotekelezwa ambayo Tanzania inanufaika ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa majitaka Mwanza na Mradi wa kikanda Usalama na Uokoaji katika Ziwa Victoria. Miradi inayotafutiwa fedha ni pamoja na upanuzi wa mradi wa majitaka katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, miradi ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na ushirikiano wa kikanda.

Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Stephen Byabato (Mb).

About the author

mzalendoeditor