Featured Kitaifa

JE, SERIKALI IMEJIPANGAJE KUONGEZA TIJA KWENYE SEKTA YA KILIMO NA KUIMARISHA SOKO LA BIDHAA? “MBUNGE MBEYA VIJIJINI”

Written by mzalendoeditor

Na Saida Issa,Dodoma

NAIBU Waziri wa kilimo David Silinde amesema kuwa Serikali kupitia Soko la Bidhaa inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuzalisha kwa tija na kuuza katika soko rasmi (Soko la Bidhaa Tanzania) ambalo litawakutanisha na wanunuzi wakubwa wa nje na ndani ya nchi na kuwapatia bei zenye ushindani.

Hayo ameyaeleza Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge Mbeya Vijijini Oran Njeza alipouliza Je, Serikali imejipangaje kuongeza tija kwenye Sekta ya Kilimo na kuimarisha soko la bidhaa.

Alisema kuwa Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kwenye Sekta ya kilimo kwa nia ya kuongeza tija kwenye uzalishaji kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo, utafiti, huduma za ugani, matumizi ya sayansi na teknolojia na kurasimisha Sekta ya kilimo mazao.

“Mheshimiwa Spika, Vilevile, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko; kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji kwa lengo la kutangaza bidhaa na maeneo ya uwekezaji katika sekta ya kilimo; kushirikiana na Sekta Binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya masoko,

kuimarisha mifumo ya kielektroniki ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo rasmi cha intelijensia ya masoko ya mazao ya kilimo (Agricultural Market Intelligence and Data Centre) ambayo itawezesha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakati, kutoa mafunzo kuhusu kilimo biashara kwa Maafisa Ugani na wakulima na kuendelea kufungua masoko mapya katika nchi mbalimbali kwa kufanya tafiti za mahitaji kwa nchi husika,”alisema.

Aidha, Serikali kupitia Soko la Bidhaa inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuzalisha kwa tija na kuuza katika soko rasmi (Soko la Bidhaa Tanzania) ambalo litawakutanisha na wanunuzi wakubwa wa nje na ndani ya nchi na kuwapatia bei zenye ushindani.

About the author

mzalendoeditor