Watu tisa wamefikiswa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza na kusomewa shtaka la mauaji katika kesi namba 2665/2024.

Akisoma shtaka hilo Februari 5,2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Juma Mpuya, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, George Ngemura aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mkazi wa Igoma jijini Mwanza, Julias Joseph ‘Bwashee’ (22), na Paul John ‘Doyi’ (23)

Wengine ni Mkazi wa Mtaa wa Mwananchi jijini humo, Leonidas Juma Bukwimba (19) na Mkazi wa Nundu jijini humo, Abdallah Hassan (31) maarufu kama ‘Dula’.

Wakili huyo pia aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Edward Boniface, miaka 19, mkazi wa Mahina, Mussa Robart, miaka 22, fundi magari, mkazi wa Ilemela Kanisani, George Mang’era Koloso, miaka 50, mfanyabiashara, mkazi wa Nyegezi, Emmanuel Makubi, miaka 21 na Charles Chacha kwa jina maarufu Ryoba, miaka 27, mkazi wa Mahina kati.

Wakili Ngemura aliiambia Mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 15, 2024 huko Mtaa wa Mwananchi, kata ya Mahina, wilayani Nyamagana kwa kumuua mlinzi, Yumen Elias (54) kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kukosa Mamlaka Kisheria ya kusikiliza shauri hilo kisha kurejeshwa rumande.

Taarifa ya kukamatwa kwa washtakiwa hao, ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Wilbrod Mutafungwa Januari 22,2024, baada ya kutiwa mbaroni na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Nyamagana Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Manyanda akiwa na timu ya makachero.

Hakimu Mpuya aliahilisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2024 kwa ajili ya kutajwa.

Previous articlePATA HABARI MOTO MOTO KATIKA MAGAZETI YA LEO FEBRUARI 6,2024
Next articleWAWILI MBARONI KWA TUHUMA ZA KULA NJAMA NA KUTAKA KUIBA MAFUTA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here