Featured Kitaifa

SERIKALI KUANZISHA SOMO LA UCHAMBUZI WA MICHEZO VYUONI

Written by mzalendo

Na Shamimu Nyaki

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inakusudia kuanza kufundisha somo la Uchambuzi wa Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo-Malya na Vyuo vingine kwa kuzingatia uhitaji wa somo hilo nchini ili kuongeza ajira na utaalamu katika eneo hilo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma Februari 1, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa jimbo la Mlalo, Lushoto Mhe. Rashid Abdallah Shangazi aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuendeleza wachambuzi wa soka nchini ili wawe na utaalamu wa kutosha katika kazi hiyo.

“Uchambuzi katika michezo ni sehemu ya mada zinazohusiana na michezo husika ambazo zipo katika sheria zinazotawala michezo. Serikali itaangalia mahitaji ya soko katika kipindi cha kuhuisha mitaala na kuzingatia eneo la uchambuzi ambalo sasa limeiletea heshima michezo kupitia wachambuzi nguli na mahiri waliopo” amesisitiza Mhe. Mwinjuma.

Ameongeza kuwa somo hilo la uchambuzi halitahusisha soka pekee bali pia michezo mingine ikiwemo Ngumi ambayo ni miongoni mwa michezo inayotangaza vyema Taifa la Tanzania na kutoa ajira.

Aidha, Mhe. Mwinjuma ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wa Michezo wapate elimu ya michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya ambacho kinatoa elimu ya ufundishaji michezo, uongozi na utawala katika michezo, elimu ya viungo vya mwili katika michezo pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, mpira wa kikapu, riadha na mpira wa wavu.

About the author

mzalendo