Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATOA BILIONI 1 KUGHARAMIA WATOTO 20 WA SELIMUNDU

Written by mzalendoeditor

NA: WAF, Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema katika kuendelea kuboresha huduma za afya nchini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha zenye thamani ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kutibu watoto 20 wenye ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) mpaka kufikia Juni 2024.

Waziri Ummy amesema hayo Leo Februari 1, 2024 wakati wa ziara ya Rais Samia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, ambapo aliwajulia hali watoto waliopandikizwa uroto katika Hospitali hiyo.

“Hatua hii inaonyesha dhamira ya serikali katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa watu wenye magonjwa maalum kama ugonjwa wa Selimundu ambapo hadi kufikia sasa jumla ya watoto watatu wameshapandikizwa uroto”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameongeza kuwa jitihada za Serikali katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalum katika jamii zinaonesha azma thabiti ya kuimarisha huduma za afya na ustawi wa wananchi kwa kutoa fedha kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa mbalimbali ambapo Serikali inaonyesha kujali na kuthamini maisha ya raia wake, hasa wale walio katika mazingira magumu ya kiafya.

Aidha, ameongeza kuwa hatua hiyo inatoa ishara ya uongozi mathubuti wa Rais Samia wa kujali na kuwajibika, ambao unazingatia mahitaji ya wananchi wake.

“Rais Samia amewezesha upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali yake katika kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa jamii”. Amesema Waziri Ummy.

About the author

mzalendoeditor