Featured Kitaifa

KAMISHNA MUSA NASSORO KUJI JUMA:GALACHA WA MASUALA YA FEDHA ANAYEIONGOZA TANAPA

Written by mzalendoeditor

Na. Catherine Mbena, Arusha

Linapotajwa jina la Musa Nassoro Kuji Juma, wasomi na wanataaluma wa tasnia ya fedha ndani na nje ya Tanzania hukubali kuwa yeye ni galacha na mbobevu wa hali ya juu.

Ana ujuzi wa kiufundi, kivitendo na uzoefu katika kushughulikia masuala ya fedha. Pia, ana ufahamu wa sasa juu ya mabadiliko na mwenendo katika sekta ya fedha, sheria na maadili katika tasnia ya nzima ya fedha nchini.

Historia yake inaturudisha hadi mwaka 1991 alipoajiriwa katika TANAPA kama Mhasibu.

Kutokana na umahiri wake katika kutekeleza majukumu aliyopewa, katika kipindi cha miaka miwili tu baada ya kuajiriwa alipandishwa cheo toka Mhasibu Daraja la II na kuwa Mhasibu Daraja la I.

Aliendelea kupandishwa vyeo na kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali hadi kufikia cheo cha Naibu Kamishna wa Uhifadhi akisimamia Kurugenzi ya Huduma za Shirika mnamo mwaka 2019. Hadi sasa Kamishna Kuji amefanya kazi katika Shirika la TANAPA kwa kipindi cha miaka 33.

TANAPA, likiwa Shirika la Uhifadhi na Utalii la Serikali linalosimamia Hifadhi za Taifa 21, na kuchangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni zinazopatikana katika sekta ya utalii hapa nchini kila mwaka.

Taarifa ya Januari 11, 2024 kutoka Ikulu inasema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemteua Kamishna Musa Nassoro Kuji Juma, mbobezi wa masuala ya fedha, kuwa Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Shirika lenye sifa kubwa nchini na duniani kwa ujumla.

Kamishna Kuji ana Shahada ya Biashara ya mwaka 1991 katika masuala ya uhasibu (Bachelor of Commerce in Accountancy) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar Es Salaam).

Mwaka 2006 alifuzu masomo ya juu ya taaluma ya uhasibu ya CPA(T). Aidha, mwaka 2014 alihitimu masomo ya Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara (Master’s in Business Administration) kutoka Chuo kikuu cha Maastricht kilichopo nchini Uholanzi (Netherlands) kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi cha Kusini na Mashariki mwa Afrika (ESAMI) kilichopo Jijini Arusha, Tanzania.

Kamishna Kuji ana rekodi nzuri ya kukuza biashara na kutoa huduma bora za utalii hususan kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya utalii nchini.

Ni mtu wa kawaida, msikivu, mwenye ufahamu mpana, anayeweza kushawishi, muwazi, mwenye mtazamo wa kukua, mwenye maadili na maamuzi yanayoliletea Shirika tija.

Kwa mfano, akiwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi akisimamia Kurugenzi ya Huduma za Shirika ambapo Shirika limekuwa likipata hati safi za ukaguzi wa fedha kutokana na umakini wake katika kusimamia taratibu za fedha, sheria za kodi na miongozo mingine ya mapato na matumizi.

Aidha, akiwa Mkurugenzi wa Fedha, TANAPA imekuwa ikipata tuzo za ushindi wa uandaaji wa hesabu kwa viwango vya kimataifa vya uhasibu kwa sekta ya umma.

Alionesha kiwango cha juu cha ufahamu wa kifedha, akiweka mikakati ya kuboresha usimamizi wa rasilimali fedha na mifumo ya mapato, ubunifu ulioliongezea Shirika mapato.

Ameendeleza mipango ya kifedha inayolingana na malengo ya Shirika. Aidha, amekuwa kiungo mchezeshaji muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kuchangamkia fursa zinazojitokeza.

Kupitia maamuzi yake yenye busara, Kamishina Kuji amevuka changamoto nyingi, akichangia ukuaji na utulivu wa TANAPA kifedha.

Maamuzi yake ya kimkakati yamelikinga Shirika sio tu kwenye afya ya kifedha, bali pia yameiweka TANAPA katika mafanikio endelevu katika miaka ijayo.

Uongozi wake umechochea ushirikiano, ubunifu, na dhamira ya pamoja ya kufanya vizuri, hivyo kuchangia mafanikio ya timu na kufikia malengo ya Shirika.

Licha ya kutokuwa na uhakika wa kiuchumi kama wakati wa kipindi cha UVIKO-19, Kamishna Kuji ameonesha ukomavu wa kustaajabisha.

Wakati Shirika linapitia katika mazingira yasiyotabirika ya kifedha, Kamashna Kuji ameshirikiana na viongozi wengine wa Shirika kwa ustadi na nguvu katika kutoa ushauri chanya.

Ustawi wa Taifa kiuchumi kupitia TANAPA ni kielelezo cha jitihada, ujuzi na juhudi zisizochoka za Kamishna Kuji.

Shirika lilikuwa na bahati ya kuwa na Mkurugenzi wa Fedha siyo tu aliyekidhi, bali pia aliyezidi matarajio. Matunda yake yanaonekana na bila shaka yataendelea kuonekana katika Shirika la TANAPA, sekta nzima ya uhifadhi na utalii na Taifa kwa ujumla.

Kutokana na uchapakazi wake, Oktoba 3, 2023, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akamteua Kamishna Kuji kuwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA na kisha mnamo Januari 11, 2024, Mhe. Rais akamteua tena kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA.

Huyo ndiye Musa Nassoro Kuji Juma, Galacha Mbobevu wa masuala ya fedha na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, ambaye ni fahari kwa Taifa.

Pongezi za dhati kwake kwani mafanikio endelevu kwa TANAPA na sekta ya uhifadhi na utalii yanatarajiwa kupatikana chini ya uongozi wake mahiri ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoitaka sekta husika kuvutia watalii milioni 5 watakaoliingizia Taifa Dola za Kimarekani bilioni 6.6 (16.5 trilioni) ifikapo mwaka 2025.

About the author

mzalendoeditor