Featured Kitaifa

MRADI WA KUPELEKA UMEME WA GRIDI RUKWA UMESHAANZA- MHE. KAPINGA

Written by mzalendo

 Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akijibu maswali mbalimbali ya Wabunge, bungeni jijini Dodoma tarehe 1 Februari, 2024.

Dodoma,

Katika jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika, Serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa wa Rukwa kupitia mradi  wa TAZA ulioanza kutekelezwa
mwezi Novemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya
upatikanaji umeme wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.

Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO inaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo na kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini amesema kuwa, upungufu wa umeme unaendelea kupungua akitaja takwimu kuwa, upungufu umepungua
kutoka megawati 400  hadi 144 kwa siku ya leo.

Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali  ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme nchini akitolea mfano utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao inatarajiwa kuwa, katika  mwezi wa Pili Kuelekea mwezi wa Tatu mwaka huu, utaanza kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

Mhe. Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi  mkoani Katavi ambapo ameeleza kuwa, tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa na kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo, nguvu  sasa inawekwa zaidi  katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenda mkoani humo.

About the author

mzalendo