Kitaifa

WATAALAMU WA AFYA WAASWA KUONGEZA UWAJIBIKAJI KUZUIA VIFO VYA UZAZI

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imewaasa wataalamu wa afya waliopata mafunzo ya Kadi Alama ya Jamii (Community Score Card) yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya ya mama na Mlmtoto mkoani Tabora kuongeza uwajibikaji ili kuzuia vifo vya uzazi.

Mafunzo hayo yanatolewa kupitia Mradi mpya wa Tanzania Maternal and Child Health Investment Program (TMCIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unaolenga kusaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini kwa kutumia Kadi Alama ya Jamii ili kufanya tathmini ya huduma husika.

Akifunga mafunzo hayo Januari 20, 2024 mkoani humo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa Ofisi hiyo, Dkt. Paul Chaote, amesema ni wakati sasa kwa wataalam hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuondoa kabisa au kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, kushughulikia malalamiko na kuongeza umiliki wa jamii kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, Dkt. Chaote ametoa wito kuifanya kadi alama ya jamii kuwa endelevu kwa kutumia bajeti za Halmashauri zao lakini pia kuwa na weledi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania.

Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa amesema mafunzo hayo yataboresha ushiriki wa jamii kwenye maeneo yao kwani itasaidia kupunguza changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi na Watoto wachanga na kuanza mara moja utekelezaji wake ili kutatua changamoto zilizopo baina ya wataalam na jamii.

Naye, Mratibu wa Elimu kwa Umma Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Robert Migango aliishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya kwa kuwapa mafunzo na kuahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote kwa vitendo katika maeneo.

 

About the author

mzalendo