Featured Kitaifa

SERIKALI KUIMARISHA HALI YA LISHE KWA VIJANA BALEHE NCHINI

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuimarisha na kuwekeza kwenye Afya za vijana balehe hasa katika hali za Lishe, Afya ya Akili pamoja na elimu ili kujikinga na magongwa yakuambukiza ikiwemo VVU/UKIMWI ikiwa ni kipaumbele cha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Tano la Kisayansi kuhusu masuala ya vijana balehe (15-19) lenye lengo la kujadili namna ya kubadili Tafiti za Afya kwa Vijana wa rika balehe na Lishe kuwa za vitendo.

“Vijana hawa balehe wana changamoto nyingi ikiwemo ya masuala ya lishe, Afya ya Uzazi, Afya ya Akili, lakini pia vijana wengi wanakabiliwa na upungufu wa damu kwa asilimia 38-40, uzito mkubwa, uzito mdogo pamoja na ukosefu wa vitamini.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema, Kangamano hilo limekutanisha wanasayansi mbalimbali kutoka Afrika, Marekani na Ulaya ili kujadili kwa pamoja ni vipi Tanzania itaweza kutumia Tafiti za Kisayansi katika kufanya maamuzi ya kisera pamoja na masuala ya Afya ya Uzazi.

“Katika Kongamano hili pia tumeona kuzinduliwa kwa utafiti ambao umeonesha kwamba, endapo wakina mama wajawazito watapewa madini ya ‘calcium’ tunaweza tukapunguza kifafa cha mimba kinachochangia vifo vya kina mama wajawazito.” Amesema Waziri Ummy

Aidha Waziri Ummy amesema, utafiti huo umeonesha badala ya kuwapa dozi ya Mg 1,500 kwa siku hata wakipewa dozi ya Mg 500 kwa siku inaweza kusaidia matokeo mazuri kwa kinamama wajawazito kutopata kifafa cha mimba ambapo pia itapumguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Mwisho, Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania ikiwemo vijana kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji kwa kupunguza mafuta, chumvi na Sukari pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka Magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa vijana nao wanakabiliwa na magonjwa hayo.

About the author

mzalendoeditor