Featured Kimataifa

MAKAMU WA RAIS ATETA NA YARA INTERNATIONAL

Written by mzalendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA wakiongozwa na Rais ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Svein Tore Holsether. Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi. Tarehe 17 Januari 2024.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA Bw. Svein Tore Holsether pamoja na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi. Tarehe 17 Januari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango akiagana na Rais ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA Bw. Svein Tore Holsether mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi. Tarehe 17 Januari 2024.

………………………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wSa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA wakiongozwa na Rais ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Svein Tore Holsether, mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi.

Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameihakikishia kampuni hiyo kwamba serikali itaendelea kuiunga mkono katika kufanya shughuli zake nchini Tanzania. Amesema dhamira ya serikali ni kuendelea kujidhatiti katika kuwa ghala la chakula kikanda kwa kuzingatia ongezeko la watu pamoja na mahitaji ya chakula.

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongeza ushirikiano zaidi baina ya kampuni hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya kilimo kama vile maghala, usafirishaji pamoja na umwagiliaji. Pia amesema ushirikiano unahitajika katika kuimarisha kilimo endelevu ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa na udhibiti wa maji.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kampuni ya kimataifa ya YARA inaweza kushirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo wakulima wadogo ili waweze kufanya kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji. Pia amewakaribisha kushirikiana katika tafiti za kilimo, kufanikisha masoko ya mazao ya wakulima na kuongeza ushirikiano na wakulima na vyama vya ushirika na taasisi zingine ili kufanikisha jitihada zilizopo.

Kwa upande wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA imesema inaunga mkono ajenda ya Afrika ya 2030 ambapo tayari imeweka mkakati wa kushirikiana na mataifa mbalimbali yenye mpango wa muda mrefu katika kuimarisha usalama wa chakula ikiwemo Tanzania. Kampuni hiyo imedhamiria kuongeza uwekezaji nchini Tanzania na kuongeza ushirikiano katika kuwajengea uwezo wakulima. Tayari kampuni hiyo inashirikiana na Mpango wa kukuza kilimo nyanda za juu kusini (SAGCOT) katika kupima afya ya udongo nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba pamoja na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva Balozi Abdallah Possi. Kwa upande wa Kampuni ya kimataifa ya YARA mazungumzo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa YARA kwa Afrika na Asia Fernanda Lopez Larsen.

Kampuni ya Kimataifa ya YARA huzalisha na kusambaza mbolea, viatilifu vya kilimo pamoja na kuwajengea uwezo wakulima.   

About the author

mzalendo