Uncategorized

TARURA YAIFUNGUA MSOMERA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Handeni

Jumla ya Km.186 za barabara zimekamilika kuchongwa na kilometa 24 zimewekewa changarawe kati ya Km. 986 za mtandao wa barabara katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Wilaya ya Handeni Mhandisi Judica Makyao wakati ya ziara ya Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff katika kijiji cha Msomera.

Ameeleza kuwa kazi ya kufungua barabara zinaendelea kwa awamu ambapo Kilometa hizo zinajumuisha maeneo ya mashamba, huduma za kijamii pamoja na makazi yaliyojengwa katika eneo la mradi huo.

“Kazi hizi zimekua zikifanyika kwa awamu na kwa sasa wakandarasi wapo kazini wanaendelea na ufunguzi na uchongaji wa barabara pamoja na ujenzi wa Makalavati 10 kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi na maeneo mengine”. Alisema Mhandisi Makyao.

Katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu huyo Mhandisi Victor Seff alisema TARURA itaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha ujenzi wa barabara katika kijiji hicho unakuwa wa viwango vilivyokusudiwa ili kufikia adhima na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Mhandisi Seff alimpongeza Msimamizi wa ujenzi wa mradi huo Kanali Sadick Mihayo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya ujenzi wa makazi ya wafugaji wanaohamia kijijini Msomera.

Naye, Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa Makazi ya Wafugaji Kanali Sadick Mihayo amempongeza Mhandisi Seff kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na watendaji wa TARURA-wilaya ya Handeni na kumpongeza Meneja wa TARURA-Wilaya ya Handeni Mhandisi Judica Makyao kwa kujitoa kwake kikamilifu ili kuhakikisha barabara zinafunguliwa na kupitika katika eneo la mradi.

Kanali Mihayo alieleza eneo la mradi linahusisha Halmashauri tatu za Wilaya za Handeni, Kilindi na Simanjiro na kuwa utekelezaji rasmi wa ujenzi wa nyumba za Makazi umeanzia katika eneo la Msomera, Wilaya ya Handeni na kwa sasa takribani barabara zote muhimu zimefunguliwa na TARURA.

Kanali Mihayo alisema kwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba utakaofanyika katika Wilaya ya Kilindi na Simanjirio kwa sasa wataamu wa kupanga matumizi ya ardhi “Surveyor” wanaendelea na zoezi la kuzitambua barabara katika eneo la Kilindi na Simanjiro ili ziweze kufunguliwa na kuendelea na ujenzi.

About the author

mzalendo