Na WAF – Dodoma.
Serikali imewataka waganga na wadau wa tiba Asili nchini kusajili dawa wanazotengeneza ili ziingizwe katika mfumo wa hospitali na kuongeza masoko ya huduma jumuishi za Afya kwa kufuata mfumo rasmi wa muongozo wa dawa.
Wito huo umetolewa leo Januari 4, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba asili Dkt. Marko Hingi wakati alipomuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu katika kikao cha waganga pamoja na wakuu vyama vya tiba asili na tiba mbadala Jijini Dodoma.
Katika kuendelea kuimarisha kada ya tiba asili amesema Serikali imeingiza baadhi ya dawa za tiba asili katika huduma jumuishi za Afya kwa kufuata mfumo rasmi wa muongozo wa dawa.
“Mpaka sasa Hospitali saba nchini zimeanza kutumia dawa za tiba asili na mbadala kama Huduma jumuishi za Afya kusaidia wananchi katika kupona magonjwa mbali mbali”. Amesema Dkt. Hingi.
Dkt. Hingi amesema kuwa ujenzi wa kiwanda cha NIMR Mabibo umefikia asilimia 98 na unatarajia kukamilika mapema mwaka huu.
“Kiwanda hicho kitakuwa ni jukwaa la uzalishaji wa dawa za tiba asili na mbadala hapa nchini na kusambazwa katika nchi za ukanda wa SADC“. Ameeleza.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Waganga wa Tiba Asili na Mbadala Prof. Hamisi Malebo amesema wana jukumu la kuondosha na kutibu magonjwa mbalimbali katika jamii, kuleta amani na kuisaidia Serikali kuifikia jamii.