Bukombe – Geita
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza na kuwashukuru Walimu wote wanaofundisha shule za Msingi na Sekondari wilayani Bukombe kwa kuwajali wanafunzi na kuwafundisha kwa weledi na maarifa ambayo yamepelekea wilaya hiyo kuwa na ufaulu mzuri.
Dkt. Biteko ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kabuhima, Kata ya Uyovu wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu za ziara zake kwenye maeneo mbalimbali katika Jimbo la Bukombe.
“ Nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Walimu wote katika wilaya ya Bukombe, wametupa heshima kubwa, miaka ya nyuma ambayo ni 2015 kurudi nyuma, hata tulipokuwa tukipangwa kimkoa katika matokeo ya Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita tulikuwa katika nafasi ya mwisho, leo Walimu wa wilaya yetu wamefanya kazi kubwa, wametuheshimisha kwani katika Mkoa kama hatuwi wa kwanza, basi tunakuwa wa Pili.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, ufaulu huo mzuri unatokana na walimu hao kuwajali Wanafunzi, kuwafundisha vizuri na hivyo kupelekea wanafunzi hao kufanya vizuri katika mitihani yao, hivyo amesisitiza suala la wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule na wasiwavunje moyo pale wanapoona hawafanyi vyema katika masomo.
Aidha, Dkt. Biteko amekea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kutopeleka watoto shule kwa nia ya kuwaozesha na kupata mahari, amesema kuwa Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan amejenga na anaendelea kujenga shule za ngazi mbalimbali nchini hivyo wajibu wa wazazi ni kupeleka watoto shule na siyo kuwakwamisha.
Katika Kata hiyo ya Uyovu, Dkt. Biteko amesema kuwa, miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa Shule za msingi na Sekondari, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na ujenzi wa taa za barabarani utakaoanza mwezi Januari mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais, Dkt. Samia aliyoitoa kwa wakazi wa Kata hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amezindua wodi mpya katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Charles Kulwa iliyoko Runzewe wilayani Bukombe ambapo wodi hiyo ni maalum kwa ajili ya kuhudumia wanawake wajawazito wanaofanyiwa upasuaji.
Akiwa hospitalini hapo, Dkt. Biteko alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1992 ikiwa kama Zahanati, mwaka 2005 ilipanda hadhi ya kuwa Kituo cha Afya na mwaka 2020 ilipandishwa hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya, ambapo aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo inayohudumia wagonjwa takribani elfu 72 kwa mwaka.
Awali, akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ambaye alikuwa mgeni maalum, alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kuinua sekta Afya katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine nchini akitolea mfano ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.
Aliwataka wadau wengine kuiga mfano wa wamiliki wa hospitali hiyo kwa kuhudumia wagonjwa wengi na kutoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu hadi kufikia hatua ya kupandishwa hadhi.