Kitaifa

SERIKALI YATOA MISAADA YA KIBINADAMU KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KILIMANJARO

Written by mzalendo

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi misaada ya kibinadamu kwa baadhi ya waathirika wa mafuriko wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maeneo yaliyoathirika katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akitembelea na kukagua baadhi ya nyumba ziliozoathirika na mafuriko wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Amir Mkalipa akitoa taarifa ya Maafa katika Wilaya hiyo wakati ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili katika Wilaya hiyo kukabidhi misaada ya kibinadamu kwa baadhi ya waathirika wa mafuriko mkoani Kilimanjaro.

Na Mwandishi wetu- Kilimajaro

Serikali imetoa misaada ya vyakula, magodoro, ndoo, madumu na mablanketi kwa kaya 119 za Kata Nane za Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro zilizokumbwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akikabidhi misaada hiyo amabyo ni mahindi tani 20, magodoro 150, mablanketi 300, ndoo 150, madumu 150, na mikeka 300 Naibu Waziri Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali inatambua changamoto iliyowakumba wananchi hao kutokana na mvua zilizonyesha na kusababisha mafuriko.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa baadhi ya watu wanaotoa taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii kucha mara moja tabia hiyo kwani wanasababisha taharuki.

“Inapotokea taarifa za maafa wapo wasemaji wake kwa mkoa ni Mkuu wa mkoa na wilaya ni Mkuu wa wilaya sasa wapo watu wanarekodi na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao na kusababisha taharuki kubwa niwaombe achaneni na hii tabia tumieni mitandao vizuri,” Alisema Naibu Waziri Ummy.

Vile vile Naibu Waziri huyo ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi kukutana na kamati ya maafa ya Wilaya pamoja na wataalam wengine ili kuweka mikakati ya uzibuaji wa njia za mto Nanga na mto Manguvu ili kuzuia mafuriko katika Kijiji cha Saningo, Kata ya Old Moshi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi alitumia nafasi hiyo kuishikuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo wamezikimbilia familia za waathirika wa mafuriko katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Prof. Ndakidemi alisema kuwa, katika maafa hayo yaliyosababishwa na mvua jumla ya watu watano walifariki dunia pamoja na mashamba na vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kusombwa na mafuriko.

“Msaada uliotolewa na serikali utasaidia kuzifariji familia ambazo zimekumbwa na mafuriko pamoja na kuwafariji watu ambao ni waathirika hatua hii ni kuonyesha jinsi ambavyo Serikali inawathamini” Alisema Prof. Ndakidemi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Amir Mkalipa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi aliutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanagawa vitu hivyo kulingana na maelekezo ya serikali na yeyote atakayekiuka hatosita kumchukulia hatua.

Kwa upande wao waathirika waliishukuru Serikali kuwajali wananchi wake wakati wote wanapokumbwa na changamoto hatua ambayo huwapa faraja na kusaidia kurejesha hali.

About the author

mzalendo