Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi tani 27 za mahindi, magodoro 250, mablanketi 700, mikeka 316 ndoo 194 na madumu ya maji 62 kwa Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Same ili kuzigawa kwa waathirika wa mafuriko katika Kata za Makanya na Hedaru zilizopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro zilizoathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akitembelea baadhi ya nyumba zilizoathirika na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Bw. Same, Sixbert Sarmett akiwasilisha taarifa ya Maafa ya Wilaya ya Same wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili mkoani Kilimanjaro kutembelea na kukabidhi misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko.
Mkazi wa Kata ya Makanya Bw. Said Faraji Islam (wa kwanza kulia) akieleza namna alivyoathirika na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili mkoani Kilimanjaro kutembelea na kukabidhi misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko hayo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Na Mwandishi wetu – KILIMANJARO
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewapongeza Wakuu wa Mikoa ambayo imekumbwa na mafuriko nchini kwa jinsi walivyojitoa kuhakikisha wanawasaidia waathirika wa maafa hayo.
Mhe. Ummy alitoa kauli hiyo wakati alipowatembelea waathirika wa mafuriko wa Kata za Makanya na Hedaru zilizopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kukabidhi misaada ya kibinadamu ambayo ni mahindi tani 27, magodoro 250, mablanketi 700, mikeka 316 ndoo 194 na madumu ya maji 62 katika kaya 159 zenye wanakaya 562 waliothirika.
Alisema kuwa, maafa ni ya kila mtu na ni jambo linalohitaji nguvu ya pamoja kupambana nalo huku akizipongeza kamati za maafa za mikoa na wilaya kwa jinsi zilivyoshirikiana na wananchi kupambana na maafa yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Serikali imeona jitahada kubwa ambazo zimechukuliwa na wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao imekumbwa na mafuriko na hili limewezekana kutokana na kufanyiwa kwa marekebisho ya sheria ya maafa mwaka jana,” Alisema Naibu Waziri Ummy.
Aidha Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalam wakiwemo watabiri wa hali ya hewa ili kuepuka maafa zaidi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Same Bw. Sixbert Sarmett alisema kuwa, mafuriko katika Kata ya Hedaru yalitokea Novemba 24 mwaka huu wakati Kata ya Makanya yalitokea Disemba 7 mwaka huu ambapo yalisababisha vifo vya watu wawili na miundombinu ya barabara kuharibika pamoja na mazao kuharibiwa.
“Mafuriko hayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa mazao ambapo hekari 423 zimeharibika pamoja na maji kuingia katika makazi ya watu na kuharibu samani za ndani ambapo kaya 256 ziliathirika.
Aidha Diwani wa Kata ya Hedaru Mhe. John Kindoli alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kupanua daraja la Hedaru pamoja na kuongeza mfereji wa kupitishia maji ili kuruhusu maji kupita kwa wingi hatua itakayosaidia kuzuia kusambaa katika makazi ya watu.
Nao baadhi ya wakazi wa Kata ya Hedaru, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mkubwa alioutoa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama.