Uncategorized

KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI CHAPIGA STOP MAGARI MABOVU

Written by mzalendo


Na Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kimesema kinaendelea na ukaguzi wa magari ya Shule ikiwa ni utaratibu wao wa kila mwaka kabla ya muhula wa masomo kuanza ambapo kimekuwa kikifanya ukaguzi wa magari hayo ili kubaini changamoto na kutoa maelekezo ya matengenezo ya vyombo hivyo ambavyo ni mahususi kwa kubeba Watoto wa Shule mbalimbali katika Mkoa huo.

Akiongea katika ukaguzi unaoendelea katika ofisi za kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mkuu wa kikosi hicho mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema kikosi hicho kimekuwa na utaratibu wa ukaguzi wa magari ya wanafunzi kabla ya shule kufunguliwa huku akibainisha kuwa lengo la ukaguzi huo ni kuweka mazingira salama kwa Watoto wanaotumia vyombo hivyo Kwenda shule.

SSP Zauda ameongeza kuwa zoezi hilo linafanyika Mkoa mzima wa Arusha huku akiwataka wamiliki na madereva kuitikia wito wa ukaguzi wa vyombo hivyo ambapo amesema wataendelea kukagua na kutoa elimu kwa madereva hao ambao wanatumia vyombo hivyo kubeba wanafunzi.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo hivyo kufanya matengenezo na ukaguzi wa vyombo vyao mara kwa mara huku akiwata wazazi na walezi kufuatilia mwenendo wa magari yanayobeba Watoto wao ilikubaini changamoto wanazopitia katika matumizi ya vyombo hivyo.

Kwa Upande wake mkaguzi wa magari, Mkaguzi msadizi wa Polisi Goodluck Banele amebainisha kuwa katika ukaguzi unaoendelea kufanyika kikosini hapo ambapo wamebaini changaoto mbalimbali ambazo zinazovikabili vyombo hivyo.

Nao baadhi ya wamiliki wa shule wamesema Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kimefanya ukaguzi huo kwa wakati sahihi ambapo shule zikiwa bado hazijafunguliwa ili kuondoa usumbufu wa ratiba za ukaguzi wakati wa masomo ukiwa umeanza huku wamiliki hao wakipongeza kikosi hicho kwa utaratibu huo wa kila mwaka.

Raphael Gunda ambae ni dereva wa magari hayo ya wanafunzi amefurahishwa na kitendo hicho cha ukaguzi akisema itasaidia kupunguza ajali ambazo zinasababishwa na changamoto za kitaalam katika vyombo hivyo.

About the author

mzalendo