Featured Kitaifa

SERIKALI KUJENGA KITUO KIPYA CHA AFYA GENDABI, HANANG

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Hanang, Manyara

Serikali kupitia Wizara ya Afya kujenga kituo kipya cha Afya katika Kijiji cha Gendabi Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara ili kusaidia upatikanaji wa huduma za Afya karibu na wananchi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo kwenye ziara yake ya kutembelea na kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, upatikanaji wa dawa pamoja na kutoa pole kwa wananchi wa eneo lililoathirika na maporomoko ya matope.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya OR-TAMISEMI tutajenga kituo kipya cha Afya katika makazi mapya yaliyotengwa na Mkoa kwa ajili ya wananchi waliothirika na maporomoko hayo na tutaanza kuleta Tsh: Mil. 500.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, Fedha hizo zimetolewa na Rais Samia ili wananchi wanaopelekwa katika eneo hilo jipya la Wareti kujengwa kituo kipya cha Afya, kununuliwa Vifaa Tiba vya kutosha pamoja na watumishi.

Aidha, katika Matokeo ya ziara hiyo Waziri Ummy amesema Serikali itapeleka magari Matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ukiondoa yale yaliyonunuliwa na Rais Samia zaidi ya 900 ya mgao ambayo TAMISEMI watayapeleka.

Pia, Waziri Ummy amesema majeruhi Watano waliosalia kati ya 139 waliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara wataendelea kuhudumia kwa gharama za Serikali.

“Mmemuona wenyewe mama wa huruma, mama wa upendo Mhe. Rais Samia amekatisha ziara yake nchi za nje amekuja kwenu ili kuwa pamoja nanyi, na sisi kama Wizara ya Afya tupo tayari kutimiza mahitaji mengine yote yatakayohitaji.” Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy ametoa shukrani kwa watumishi wote walishiriki katika kazi ya kuwahudumia wana-Katesh ikiwemo Madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa usingizi, watu wa maabara, wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii na Watanzania wote kwa ujumla.

About the author

mzalendoeditor