Featured Kitaifa

SERIKALI KUWANYANYUA VIJANA KIUCHUMI NA KIMITAJI – MHE. KATAMBI

Written by mzalendoeditor

 

Na: Mwandishi wetu – Mwanza

SERIKALI imeendelea kubuni Mikakati ya kuhakikisha Vijana wanapata ujuzi na fursa za kuwainua kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao.

Aidha, Mhe. Katambi amesema kuwa Serikali kwa kutambua mchango wa vijana katika ujenzi wa taifa vijana nchini wameendelea kunufaika kwa kupatiwa mafunzo ya kuendeleza ujuzi wao, kuboresha Mwongozo wa Utoaji Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na kutenga maeneo katika Halmashauri kwa ajili ya shughuli za vijana.

Hayo yamebainishwa Desemba 27, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 15 la Umoja wa Vijana Wakatoliki wa Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu Tanzania (TMCS) Taifa, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.

Mhe. Katambi pia amewataka Vijana nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira zinazotolewa na Serikali.

Vilevile, amewasisitiza vijana wanaokidhi vigezo kuchangamkia nafasi za kazi 500, Kada ya Uuguzi kwa kutuma Maombi yao kupitia tovuti ya www.jobs.kazi.go.tz ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia pamoja na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu ajira za watanzania katika nchi hizo, mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Disemba, 2023.

About the author

mzalendoeditor