Kitaifa

UMOJA WA MABALOZI WA AFRIKA WAKABIDHI MSAADA HANANG

Written by mzalendo

Umoja wa Mabalozi wa nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania wamekabidhi msaada wa mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba kwa wananchi waliokumbwa na mafuruko na maporomoko ya udongo katika eneo la Katesh Wilayani Hanang mkoa wa Manyara.

Akikabidhi msaada huo kwa Serikali, Kiongozi wa Mabalozi hao na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed amesema kundi la Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao Tanzania lina mabalozi 24 ambao wameonesha kuguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kuona ni vyema kuwasaidia wananchi hao pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji.

Dkt. El Badaoui Mohamed amesema umoja wa Mabalozi wa Afrika nchini wameguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kwa umoja wao wamechangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo la Katesh ili kurejesha makazi ya wananchi hao.

“Tunaendelea kuomba Mungu awajalie subira na kwa wale waliopoteza maisha wapumzike kwa amani. Kadhalika, kwa waliosalia basi msaada huo utawasaidia kujenga makazi yao na kuendelea na maisha kama ilivyokuwa awali,” alisema Dkt. El Badaoui Mohamed

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Serikali amewashukuru mabalozi hao kwa umoja wao na kwa msaada huo ambao utasaidia kurejesha makazi ya wananchi wa Katesh.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa baada ya kupokelewa utaratibu utafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa ili mifuko hiyo iwasilishwe katika Kijiji cha Katesh, Wilayani Hanang.

“Tunashukuru sana kwa msaada huu, baada ya kutokea kwa maafa yale sote tunajua Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha maisha ya watu yanarejea katika hali ya kawaida. Msaada huu utasaidia katika ujezi wa nyumba zilizoathiriwa na mafuriko hayo,” alisema Mhe. Balozi Mbarouk.

Balozi Mbaorouk amesema msaada huo ni uthibitisho kwamba uhusiano kati ya Balozi zote zilizopo nchini hususan Balozi za Afrika ni mzuri na kwa msaada huo wameonesha ushirikiano mkubwa na Serikali ya Tanzania.

About the author

mzalendo