Featured Kitaifa

SHIRIKA LA AMEND LATOA MAFUNZO KWA BODABODA

Written by mzalendo

IMEELEZWA kuwa kutofahamu tafsiri sahihi ya alama za barabarani ni moja wapo ya sababu za kushamiri ajali za barabarani miongoni mwa waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda.

Hayo yalielezwa jijini hapa jana na Mratibu wa Miradi kutoka shirika la AMEND, Ramadhan Nyanza wakati wa utoaji mafunzo ya usalama barabarani na huduma ya kwanza yaliyotolewa kwa madereva bodaboda mkoani hapa.

“Madereva wengi wa bodaboda hawafahamu tafsiri sahihi ya matumizi ya alama za barabarani na ndiyo maana wamekuwa wakivunja sheria na kusababisha ajali. Akiona taa ya njao anadhani kwamba anapaswa kuongeza mwendo aweze kuvuka haraka.

“Baadhi hawajui akiwa kwenye mzunguko wa barabara anapaswa kukaa upande upi, wakati wa kulipita gari hatua zipi za tahadhari anapaswa kuzichukua. Tumeamua kuwapa mafunzo ya usalama barabarani kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa usalama zaidi,” alieleza.

Pia, alisema mafunzo hayo yamekwenda pamoja na utoaji elimu ya huduma ya kwanza kwa majeruhi wa ajali kwa sababu mara nyingi ajali zinapotokea bodaboda wamekuwa watu wa kwanza kufika katika eneo la tukio.

Mratibu huyo wa miradi alisema elimu hiyo itasaidia kupata uelewa sahihi wa namna ya kumuhudumia majeruhi kabla ya kumfikisha hospitalini kupata matibabu zaidi.

Alibainisha kuwa tayari wametoa mafunzo kwa madereva bodaboda zaidi ya 180 kutoka kata nne za Dodoma lengo likiwa kuwafikia madereva 250.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu mkoani Dodoma, Erick Msemwa, alisema wametoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva hao yatakayowawezesha kutoa huduma kwa usahihi pindi ajali inapotokea.

“Kundi hili ni muhimu kwa sababu tumeshuhudia mara nyingi ajali inapotokea wamekuwa wa kwanza kufika eneo la tukio, hivyo elimu ya huduma ya kwanza itawasaidia kuwahudumia majeruhi kwa usahihi kabla ya kuwapeleka hospitalini,” alisema.

Mnufaika wa mafunzo hayo, Ali Juma ambaye ni dereva bodaboda alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa msaada muhimu kwao kwa sababu wengi wao wamekuwa wakizipuuza alama za barabarani kwa kutofahamu tafsiri yake.

“Kuna alama zingine kumbe zinatueleza kuzingatia usalama wangu na chombo ninachokiendesha katika eneo husika, lakini sisi hatuzifahamu na ndiyo moja ya sababu zinazochangia ajali,” alieleza.

Dereva mwingine wa bodaboda ambaye ni Mkazi wa Makole, Ivan John alisema baadhi ya madereva wa bodaboda hawazingatii sheria kwa sababu hawajapitia mafunzo ya kuendesha vyombo vya moto.

Alisema mafunzo kama hayo ni muhimu kwa sababu yanasaidia kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikiighalimu serikali kwa kupoteza nguvu kazi ya taifa.

About the author

mzalendo