Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa wa Dodoma hautafumbia macho suala la wanafunzi wanaoendelea kusoma kuchelewa kuripoti shuleni kwani limekuwa likiathiri ufundishaji, ujifunzaji na ukamilishaji wa mada.

RC Senyamule ameyasema hayo leo Desemba 22,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2024 kwenye kikao kazi kazi maalum cha wataalam wa elimu na viongozi.

Amesema kwa wanafunzi ambao hawatokuwa darasani Januari 8 ,2024 bila sababu za msingi watalima matuta 10 kama utekelezaji wa mpango wa elimu ya kujitegemea na mkoa pamoja na adhabu nyingine itakayoonekana inafaa kwa mujibu wa taratibu.

“Hivyo niwasihi wazazi wasiwacheleweshe wanafunzi bila sababu za msingi na wahakikishe wanakuwa darasani kwa tarehe ya kufungua shule yaani tarehe 8 Januari,2024 na waendelee kuhudhuria, mkoa na wilaya zake utachukua hatua kali kwa wazazi ambao watoto wao hawatahudhuria shuleni (utoro),”amesema RC Senyamule.

Aidha, amewasihi wazazi kuhakikisha wanawaandaa wanafunzi vizuri kwa kuwapatia vifaa vya shule mapema ili waweze kuanza masomo yao kwa wakati, pia ametumia wasaha huo kuwalelekeza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kutekeleza maelekezo hayo kikamilifu.

Amesema katika matokea yaliyotolewa na NECTA mkoa wa Dodoma umefanya tathmini kupitia kikao cha wataalamu wa elimu kilichokaa mjini Kondoa kwa siku Nne kuchambua ufaulu wa shule na Halmashauri zake kilibainisha kuwa mkoa huo una ufaulu wa 87.5% kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la 4.4% ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo ilikuwa 83.1%.

“Katika matokeo haya kila halmashauri imeongeza ufaulu ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepanda kutoka 78.2% hadi 86.37% sawa na ongezeko la 7.92%, Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma kutoka 89.93% hadi 93.18% sawa na ongezeko la 3.25%, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kutoka 86.49% hadi 89.81% sawa na ongezeko la 3.32% na n.k,”amesema.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Ally Gugu amesema kuwa mkakati ulio andaliwa na mkoa huo utasaidia kupaisha ufaulu kwa wanafunzi na kuwa na ubora wa elimu ambayo itawasaidia kufanya vizuri.

“Kwakuanzia na mwaka ujao wa elimu tutakuwa tuna mkakati maalum wa kudhihilisha huu uwajibikaji tunao usema lakini kuwa na ubora wa elimu ambayo inatolewa katika mkoa wetu wa Dodoma, tukifanya hivyo naamini tutazidi kupaa juu katika kuhakiksha pengine tayari mkoa wetu unaweza,”amesema Gugu.

Kikao kazi hicho maalum cha wataalam wa elimu na viongozi kimeongozwa na kauli mbiu inayosema “Uwajibikaji wangu ni msingi wa kuinua ubora wa elimu ya ufaulu Dodoma 2024”.

Previous articleSHIRIKA LA AMEND LATOA MAFUNZO KWA BODABODA
Next articleDORIS MOLLEL FOUNDATION YATOA VIFAA TIBA KWA AJILI YA KUANZISHA WODI YA WATOTO WACHANGA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here