Featured Kitaifa

e-GA YAFANIKIWA KUJENGA MFUMO WA GovESB

Written by mzalendo

MKURUGENZI  Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidigitali leo Desemba 22,2023 jijini Dodoma.

MKURUGENZI  Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidigitali leo Desemba 22,2023 jijini Dodoma.

SEHEMU ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi   Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba,wakati  akitoa taarifa kuhusu mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidigitali leo Desemba 22,2023 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

 

MAMLAKA ya Serikali Mtandao(e-GA) imefanikiwa kujenga Mfumo unaowezesha mifumo  ya serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa wa (GovESB) ambao utasaidia kuongeza usalama wa taarifa.

Hayo yamesemwa leo Desemba 22,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidigitali.

“Mfumo huu umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuzingatia kifungu cha 48 (2) cha sheria ya serikali mtandao Na. 10  ya mwaka 2019 kinachoitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao kuanzisha na kuendesha mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa”amesema Mhandisi Ndomba

Mhandisi Ndomba amesema kuwa , sambamba na kutekeleza matakwa hayo ya kisheria pia ujenzi wa mfumo wa GoVESB, ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inaunganishwa na kubadilishana taarifa.

“Mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini ni mfumo wa kielektroniki unaounganisha mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma iweze kusomana na kubadilishana taarifa kila inapohitajika”amesema 

Hata hivyo amesema kuwa  lengo la mfumo huo ni kuziwezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali kwa usalama, kupunguza udurufu wa mifumo, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda kwakuwa taarifa hupatikana kwa wakati.

Aidha, amesema  kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo wa GovESB, kulikuwa na changamoto mbalimbali za ubadilishanaji wa taarifa za umma, zikiwemo kutumia muda mrefu kupata taarifa kwakuwa taasisi zililazimika kuwasilisha maombi ya kupata taarifa kwa njia ya barua.

“Utaratibu huu wa barua ulichukua muda mrefu kupata taarifa hizo jambo lililochangia kupunguza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi”amesema

Mhandisi Ndombo amesema kupitia GovESB changamoto hizo zimetatuliwa na sasa taasisi zote zinabadilishana taarifa kupitia mfumo huo kwa wakati na kwa usalama zaidi.

”Mfumo huo umesaidia kuokoa muda wa kuwahudumia wananchi, pia kupunguza gharama za kutengeneza mifuo midogo ya TEHAMA inayounganisha na mifumo ya taasisi nyingine.”amesema 

Hata hivyo, amesema hadi sasa jumla ya taasisi 109 zimeunganishwa katika mfumo huo na mifumo 117 imesajiliwa.

“Miongoni mwa taasisi hizo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Wakala wa leseni za Biashara (BRELLA) na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)”amesema

About the author

mzalendo