Featured Kitaifa

IAA YAJIPANGA KUJITANUA KITAIFA NA KIMATAIFA

Written by mzalendoeditor

Na Mwandishi Wetu Arusha 
 
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka amesema Chuo hicho kimejipanga kuongeza wigo wa kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam kitaifa na Kimataifa.
 
Prof. Sedoyeka ametoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba yake katika mahafali ya 25 ya IAA yaliyofanyika jijini Arusha.
 
“Katika Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa Chuo wa miaka mitano wa mwaka 2022/2023 hadi mwaka 2026/2027 tumejiwekea lengo la kuongeza wigo wa kutoa elimu Kitaifa na Kimataifa. Kwa sasa tuna Kampasi nne ambazo ni Arusha, Babati, Dar es Salaam na Dodoma na kuanzia mwaka 2024 tunatarajia kuanza kujenga Kampasi Mpya ya Songea mkoani Ruvuma .” amesema.

 

 

Ameongeza kuwa pamoja na mpango wa kujenga kampasi ya Songea, IAA inaendela kuboresha miundombinu ya kutoa elimu, ikiwemo madarasa, hosteli, maabara za kompyuta katika Kampasi za Arusha na Babati, na kujenga jengo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 4500 kwa mara moja kampasi ya Dodoma.
 
Aidha, amesema IAA imeanza hatua za awali za kuanzisha Kampasi ya kwanza Kimataifa inayotarajiwa kuanzishwa nchini Sudan ya Kusini mjini Juba, katika mwaka wa masomo wa 2024/2025.                  

 

 

 

 

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde ambaye aliyekuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo akimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza IAA kwa hatua hiyo, na kwa namna ilivyoboresha miundombinu katika kukidhi ongezeko la wanafunzi wa elimu ya juu ambalo ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya elimu.
 
Vile vile Mhe. Silinde ametoa wito kwa wahitimu kutumia elimu waliyopata kupambana na umaskini na kuleta maendeleo katika familia zao, jamii inayomzunguka na Taifa kwa ujumla ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa nchi pia.

 

 

Katika hatua nyingine Mhe.Silinde ametoa rai kwa wahitimu kutumia matokea ya tafiti zao kutatua changamoto za jamii, “Msifungie matokeo ya tafiti zenu baada ya kuhitimu yatumieni shirikisheni jamii ili yaweze kuwa chachu katika kuleta mabadiliko chanya, kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi na utendaji kazi wa kila siku.”
 
Dkt. Suleiman Serera (mhitimu shahada ya uzamili) ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro amesema wanafunzi wengi walivutiwa kujiunga IAA kutokana na ubunifu katika utoaji wa elimu bora; huku akiomba jamii, taasisi za umma na binafsi kutumia tasnifu walizoandika ili ziweze kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii.
 
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, CPA. Joseph Mwigune amesema idadi ya wahitimu kwa mwaka 2023 imeongezeka kutoka wahitimu 3529 mwaka 2022 na kufikia wahitimu 5387; kati yao wahitimu wa shahada ya uzamili ni 1139, shahada 1027, stashahada 1260 na astashahada 2061.

 

About the author

mzalendoeditor