Featured Makala

DAKIKA 40 CHUMBA CHA WANAOZALIWA KABLA YA WAKATI

Written by mzalendo

 

Novemba 17, 2023, Dunia iliadhimisha siku ya Mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati, siku moja kabla, nilibahatika kufika katika Wodi maalumu kwenye mojawapo ya vyumba vya kutunza Watoto hao katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na kujenga msingi wa simulizi hii.

Ni kijichuchumba kidogo chenye nafasi, makadiliyo ya mita 5 kwa 2.5 za mraba, nilikaribishwa na joto la wasitani, macho yakavutwa na vitanda mithili ya minara ya kuonesha, ngazi tatu kila kimoja, ya kwanza ikihifadhi vifaa, ya pili ni kijiboksi kilichozingwa kwa kingo za plastic inayoonesha kilicho ndani, yatatu ilisimama kama paa yenye mkonga wa kusaidia kuegesha drip. 

Ndani ya viboksi ngazi ya pili kulikuwa na vichanga wakirusha miguu na mikono, kwa haraka sikufahamu ilikuwa ishara ya furaha ya kuja duniani au maumivu, jambo nililokuwa na uhakika nalo, vitendo vile vilithibitisha Uhai. 

Baadhi ya vichanga viliwekwa vifaa kwenye ngozi kufuatilia mapigo ya Moyo na upumuaji, vifaa vingine viliwekewa kwenye mguu au mkono kusoma kiwango cha Oksijeni na Joto la Mwili. 

Harakati za huduma ziliendelea, Muuguzi akimsaidia mama kukumbata mtoto katikati ya kifua chake, nikaambiwa ni ulezi-Kangaroo hufanyika kumsaidia kichanga apate joto la mama. 

Pembezoni mwa mojawapo ya vitanda hivyo, alisimama Muuguzi, mama wa kichanga akiwa kitako pembeni yake wakishirikiana kumlisha chakula kichanga kwa kutumia mpira maalumu wa kulishia. 

Ingawa, sura za kina mama waliyokuwa katika Wodi hiyo zilisawajika, macho na matamshi yao yalikuwa yenye matumaini na upendo mkubwa. 

Vichanga wale walikuwa wadogo kwa umbo na mwonekano, hawakuwa sawa na vichanga wanaozaliwa wakiwa wametimiza umri wa kukaa tumboni yaani wiki 37, hivyo walizaliwa na uzito pungufu, gram 700 hadi 900 kwa niliyobahatika kupata taarifa zao.

Ifahamike kuwa, kisayansi mtoto hupaswa kukaa tumboni kwa mama kwa takribani wiki 37, afikishe uzito wa kilo 2 hadi 3.5 ndipo akamilike kujiumba na kuwa tayari kukabiliana na hali ya Dunia. 

Hata hivyo, hali huwa tofauti miongoni mwa vichanga 13.4 ( UN 2020) wanaozaliwa kabla ya kufikisha wiki 37 kote dunia, hivyo kuzaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali  na hata kufariki kabla ya kufikisha siku 28. 

Dkt. Julieth Kabengula, Bingwa wa Magonjwa ya Watoto na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Watoto BMH, anasema Watoto hao hupitia changamoto za kiafya kwa kuwa huzaliwa kabla viungo mbalimbali havijakamilika kujiumba.  

“Hupatwa na changamoto ya upumuaji kwa sababu mapafu hayajakomaa, miili yao haiwezi kudhibiti joto hivyo mara nyingi joto hushuka chini ya kiwango na kuhatarisha uhai, na wakati mwingine hawawezi kugandisha damu, na wanaweza kupungukiwa na sukari mwilini” Dkt. Kabengula. 

Asilimia 11 ya wanawake wanaojifungua kila mwaka nchini hupata Watoto kabla ya wakati, huku vifo 50,000 vikiwakabili Watoto wenye umri chini ya siku 28 ambapo asilimia 27 ya vifo hivyo huwakabili Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati. 

Dkt. Kabengula anasema, vifo hivyo vinaweza kuepukika ikiwa Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati watapatiwa huduma mapema. 

“Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanaweza kuishi kama wengine endapo tutadhiti visababishi vinavyokatisha uhai wao, ikiwemo kudhiti sukari, joto, maambukizi na kutokwa damu” Alisema Dkt. Kabengula. 

Takwimu za BMH zinaonesha kuwa asilimia 95 ya Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati na kufikishwa kwenye Wodi maalumu ya Uangalizi Hospitalini hapo hupata nafuu na kuruhusiwa.

Hata hivyo, nilipata shauku ya kuwatafuta kina mama waliyowahi kupita katika wodi hiyo maalumu. kujionea Uso kwa Macho maendeleo ya Watoto hao baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani. 

Nilianza kwa kusafiri umbali wa kilometa 19 mwendo wa nusu saa kwa gari kwenda Mtaa wa Kikuyu hapa jijini Dodoma, huko nilimfuata Bi. Olabeth Nikanoni Martine, aliyepata Watoto mapacha kabla ya wakati. 

Hadithi ya Bi. Olabeth ni chungu tamu, kama mama yeyote alikuwa na shauku ya kupata mtoto, hata hivyo ujauzito ukawa kizungumkuti ukamlazimisha kulala kidandani hadi utakapofikisha wiki 37, lakini safari ya kulala bila kujali ugumu aliyoupata ilikoma baada ya wiki 26.  

“Niliona kitu kama maji yanatoka sehemu za siri, tukakimbia Hospitali ambako niliambiwa napaswa kujifungua, nikapelekwa chumba cha kujifungua, nikajifungua Watoto mapacha wa kike na wa kiume, watoto walikimbizwa wodi maalumu” Alisimulia Bi. Olabeth kwa Uchungu. 

Akiwa katika kilele cha furaha ya kupata watoto, ndipo habari aliyoitaka iwe, haikuwa, kama alivyotarajia watoto baada ya wiki 37 za ujauzito, akaishia wiki 26 ndivyo ilivyokuwa alipoalikwa kutambulishwa kwa wanae katika wodi maalumu (Chumba cha Joto). 

“Niliambiwa Kulwa alifariki kwa kushindwa kupumua,tumaini langu likabaki kwa Doto, lakini nilivyomwona nilishituka, niliumia kwa sababu alikuwa ni mdogo, mwenye gram 900, anayepumua kwa kutumia msaada wa mashine” Bi. Olabeth alisimulia kwa Uchungu. 

Safari, ya wiki 7 kuishi na mwanae katika Wodi maalumu ya kulelea Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati (Chumba cha Joto) ikaanza, anasema haikuwa tambarare alipanda vilima na milima, akashuka mabonde na vibonde.  

“Kuna wakati mtoto anashindwa kupumua anawekewa mashine, hawezi kula, akila tumbo linajaa, inabidi awekewe drip, anabadilika kila mara, kama mama nilikuwa nakosa nguvu” Alikumbuka Bi. Olabeth, akipepesa macho kama anayezuia machozi. 

Mkasa wa Bi. Olabeth hautatosha kwenye Makala hii pekee una ngano nyingi zilizosheheni ujasili, uvumilivu na ustahimilivu wa mama, niliachana naye na kuelekea Mtaa wa Ihumwa nje kidogo ya jiji la Dodoma mwendo wa zaidi ya kilometer 20. 

Ihumwa nilimfuata mama mwingine, Bi. Anne Mlei au mama Mikaela kama anavyopenda kuitwa, alijifungua mtoto wiki ya 29, huku akipitia changamoto nyingi wakati wa ujauzito. 

“Nilikuwa nalazwa mara kwa mara kwa sababu ujauzito ulitishia kutoka, mara ya mwisho nilikuwa kliniki, nikahisi kama kutokwa na maji, nikalazwa kwa siku tano ambapo ililazimika nifanyiwe upasuaji wa kumtoa mtoto” 

Kama ilivyokuwa kwa Bi. Olabeth, mama Mikaela alijikuta katika wakati mgumu alipokutana na Mikaela kwa mara ya kwanza. 

“Nilipoletewa mtoto wangu, nilishangaa sana, alikuwa tofauti na Watoto wengine, alikuwa ni mdogo sana, nikasema Mungu wangu nimezaa nini hiki, niliogopa mno, alikuwa tofauti na Watoto niliyozoea kuwaona” Alinisimulia Mama Mikaela kwa hisia zilioaksi kumbukizi ya siku husika. 

Pamoja na simulizi nzito, jambo nililoliona wazi na la pekee kwa Bi. Olabeth na Mama Mikaela ni upendo, Moyo wa shukrani na furaha ya kuwa na mtoto. Lakini je, kwanini mama ajifungue kabla ya wakati? 

Kwa mujibu wa Dkt. Kabengula, kuwa na maambukizi wakati wa ujauzito, lishe duni, upungufu wa damu, shinikizo la juu la damu, au sababu nyingine ikiwemo kuwa na ujauzito wenye mtoto zaidi ya mmoja ni baadhi ya visabishi. 

“Njia rahisi ya kumsaidia mama asijifungue kabla ya wakati ni kwa wanandoa kuzingatia lishe bora, kufika Hospitali mapema mama anapopata ujauzito, ili kufuatiliwa kwa karibu kwa kufanya vipimo vya damu, kutibiwa maambukizi na kudhibiti shinikizo la juu la damu” Alisema Dkt. Kabengula. 

Serikali imepiga hatua kuhakikisha huduma za Afya hasa kwa mama na Mtoto zinaboreshwa na kupatikana kote nchini, kwa kujenga vituo vingi vya kutolea huduma, kusomesha wataalamu, na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinakuwepo. 

Hatua hizo zinapunguza vifo vya Watoto kabla ya siku 28 baada ya kuzaliwa, Ushahidi wa utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania 2021-2022, unaonesha kina mama wengi wanapokea usaidizi wa kitaalamu wakati wa kujifungua kutoka asilimi 66, 2015-16 hadi asilimia 85, 2021-2022. 

Mwandishi wa Makala haya ni Raymond Mtani

Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa-Dodoma. 

About the author

mzalendo