Featured Kitaifa

DKT.DUGANGE: WAMEBAKI MAJERUHI 36 WA MAFURIKO YA HANANG WANAENDELEA NA MATIBABU

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Festo Dugange amesema idadi majeruhi wa mafuriko ya tope Hanang mkoani Manyara wanaoendelea na matibabu imepungua kutoka 117 hadi 36 na sh.milioni 560 zimetolewa kwaajili ya huduma za afya kwa wathirika hao.

Dkt. Dugange akiwa ameambatana Mhe. Jenista Mhagama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera,Bunge na Uratibu na mhandisi Godfrey Kasekenya Naibu Waziri wa Ujenzi katika ukaguzi wa maeneo yaliyoathirika ambayo serikali inayarejesha kwenye hali yake katika Mji wa Katesh wilaya ya Hanang, amesema;

“Tunauhakika hao 36 waliobahi wataendelea kuruhusiwa kurejea nyumbani kuendelea na majukumu yao na jambo la muhimu kwenye majanga haya serikali inajitahidi kudhibiti magonjwa ya mlipuko kujitokeza na sehemu kama hii tulichokifanya tumeimasha mfumo ya udhibiti wa magonjwa ya mlipuko kwenye jamii yetu na katika kambi zetu” Dkt. Dugange

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema serikali imeanza mazungumzo na taasisi za kifedha ili kutoa unafuu kwa wafanyabiashara walioathiriwa na mafuriko na ameendelea kushukru wadau wanaoendelea kutoa msaada.

Waziri Jenista Mhagama amesema kuwa mbali na Serikali kurejesha miundombinu pia imeendelea kuwa bega kwa bega na Wananchi sambamba na kutoa maagizo kwa Wataalamu wa Satellite kuanza kuangalia Kaya zote na kuona zipi zimeathirika zaidi huku ikiendelea kutoa msaada zaidi.

Aidha,Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema hadi sasa urejeshaji wa miundombinu ya barabara na makalvati yaliyoharibiwa na maporomoko ya tope na mawe yaliyotokea Desemba 3, 2023 kwenye Mji wa Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara umefikia asilimia 75.

Kasekenya amesema kazi hiyo kukagua imefanywa na Wakala ya Barabara (TANROADS) wakishirikiana na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

About the author

mzalendoeditor