Featured Kitaifa

DKT. BITEKO:TANZANIA YAPIGA HATUA UTEKELEZAJI WA AJENDA YA AFRIKA 2063

Written by mzalendo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi wakati alipofika ofisini kwake kwa ajili ya kuwasilisha salamu
za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  alipomwakilisha kwenye Mkutano wa Ajenda 2063 uliohusisha Wakuu wa Nchi za Afrika

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitoa ufafanuzi juu ya maendeleo ya utekelezaji wa Ajenda 2063 kwa Tanzania wakati wa Mjadala wa wazi uliofanyika jijini Gaborone, Botswana

Wakuu wa Nchi za Afrika wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Ajenda 2063 uliofanyika nchini Botswana. Wa pili kulia ni Rais wa Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi.

Gaborone – Botswana

Imeelezwa kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye utekelezaji wa
makubaliano ya Ajenda 2063, ya kuifanya Afrika kuwa mahali pa ndoto
yetu kuelekea Afrika tuitakayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt.
Doto Biteko kwenye Mkutano wa kujadili utekelezaji wa makubaliano
yaliyofikiwa na Wakuu wa Nchi juu ya Ajenda 2063 kwa nchi za Afrika,
alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mkutano
huo jijini Gaborone, Botswana, ulioenda sambamba na maadhimisho ya
Tamasha la KUSI.

Dkt Biteko alisema kuwa,  kimsingi Tanzania imepiga hatua kubwa katika
utekelezaji wa Ajenda hiyo ikiwemo  masuala ya amani, usalama na
demokrasia kupewa kipaumbele kwenye  nchi, kuunganisha miradi
mbalimbali ya maendeleo na nchi za Afrika ikiwemo ule wa SGR, pamoja
na miradi ya umeme kupitia nchi za Kenya, Uganda, Ethiopia, na Zambia,
na kufungua fursa za kiuchumi kwa nchi za Afrika.

“Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika itaendelea
kutekeleza, kusimamia,na kuendeleza harakati hizi za kuifanya Ajenda
hii kutimiza Dira ya Afrika tuitakayo. ” Alisisitiza Mhe. Dkt. Biteko

Ajenda ya Afrika 2063 Afrika tuitakayo imebeba vipaumbele Saba
ambavyo ni pamoja na kuleta Afrika pamoja kwenye masuala ya Maendeleo,
kuunganisha Bara la Afrika kwenye masuala ya kisiasa kwa kutumia tunu
za Afrika, Utawala  Bora na unaozingatia sheria, Demokrasia, na Haki,
Kuilinda Afrika, Afrika yenye mwelekeo wa utamaduni wake na Maadili,
Afrika itakayowaletea Maendeleo watu wake, kwa manufaa ya wanachi wa
Afrika.

Aidha Mhe Dkt. Biteko alishiriki mjadala wa Marais kutoka Afrika
kuhusu Ajenda ya umoja wa Afrika 2063 ijulikanayo kama Africas  Agenda
2063 inayotoa mwelekeo wa Afrika kutimiza ndoto zake na kuifanya
Afrika waitakayo, mjadala uliohusisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa
Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson
Mnangagwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Dkt. Edouard Ngirente
akimwakilisha Mhe. Rais, Paul Kagame, na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko, akimwakilisha Mhe. Dkt
Samia suluhu Hassan.

Katika mjadala huo Mhe. Dkt. Biteko Alitoa tathmini ya utekelezaji wa
Malengo ya Ajenda ya Afrika 2063 na tathmini ya miaka kumi ya awali
kwa Tanzania, ambapo alisema kuwa Tanzania iliridhia mikataba ya
utekelezaji wa Ajenda hiyo ya Afrika mwaka 2013 katika utekelezaji wa
dira hiyo ya Afrika  ambapo imepiga hatua kubwa katika  uanzishwaji wa
eneo huru la Biashara la Afrika na kuondoa vikwazo vya kibiashara,
watu na bidhaa kwa maendeleo ya Tanzania.

Aidha, Mhe Dkt. Doto Biteko akiwa nchini Botswana alipata fursa ya
kukutana na Rais wa Botswana na kuwasilisha salamu rasmi kutoka kwa
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Dkt. Samia Suluhu
Hassan ambapo pamoja na masuala mengine walijadili namna
watakavyoboresha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili
ikiwemo kuangalia uwezekano wa kufungua ubalozi nchini Botswana ili
kurahisisha utendaji kazi, ushirikiano kwenye masuala ya kiuchumi,
Madini, Sanaa, na Utamaduni.

Ujumbe wa Tanzania ulioongozana na Mhe. Dkt Biteko ni pamoja na Waziri
wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji
kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrick Soragha,
Mkurugenzi wa Mipango kutoka Tume ya Mipango,  Dkt. Mursali Ally
Milanzi, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi Ellen
Maduhu pamoja na  Balozi Edward Komba, Mkuu wa Utawala na Kaimu Balozi
wa Tanzania Pretoria na anayeshughulikia Botswana.

About the author

mzalendo