Featured Kitaifa

DKT. BITEKO AAGIZA WAKURUGENZI, MAMENEJA TANESCO KUKEMEA RUSHWA KWENYE MAENEO YAO

Written by mzalendo

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza katika kikao na Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa  wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kilichofanyika leo Disemba 2,
2023 jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza katika kikao
na Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kilichofanyika leo Disemba 2, 2023 jijini Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa
katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kikao  kilichofanyika leo
Disemba 2, 2023 jijini Dodoma

Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko  (katikati, mbele )katika kikao kilichofanyika leo
Disemba 2, 2023 jijini Dodoma

…………….

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya kikao kazi na Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa wa  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo katika kikao kazi hicho ametoa maagizomakuu matatu ambayo ni kupambana na rushwa katika maeneo ya kazi,
kujenga mahusiano mazuri na watu na kutekeleza maono ya vitu vitakavyoboresha utendaji kazi kwenye maeneo yao bila kuona kuwa fedha ni kikwazo cha utendaji kazi.

Amesema hayo, wakati wa kikao kazi kati yake na Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa wa TANESCO kilichofanyika tarehe 2 Disemba 2023 na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati wakiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga na Kaimu Katibu Mkuu,
Athumani Mbuttuka.

“Nendeni mkapambe na rushwa kwa watu wenu, na Watu wa Utawala mkiletewa mtu ana kosa la rushwa na kuna ushahidi mshughulikieni huyo mtu haraka, watu waridhike na wanachopata, wasichukue rushwa kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko pia amewataka Wakurugenzi na Mameneja wa TANESCO, kujenga mahusiano mazuri na watu walio chini yao, pia na viongozi mbalimbali kwenye maeneo wakiwemo wa Serikali na Bunge, akieleza kuwa Wizara ya Nishati inapaswa kuwa  Wizara inayotegemewa na kukimbilia.

Vilevile, Dkt. Biteko amewataka Wakurugenzi na Mameneja wa TANESCO, wakiwa na maono ya kubadilisha na kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao wayaseme na wayafanyie kazi  bila kuona kuwa fedha ni kikwazo cha kutekeleza maono hayo.

Amewapongeza Wakurugenzi na Mameneja TANESCO nchini kwa kazi kubwa wanayofanya katika kusimamia kazi za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ambayo ina matarajio makubwa ya wananchi na kuwakumbusha kuwa, wananchi wanachohitaji ni umeme na siyo michakato.

“ Wote nataka tufikiri tunawapaje watu umeme kwani tuna njia na nyenzo za kufanya jambo hili liwezekane ikiwemo Wataalam wa muda mrefu, wa kati na wapya ambao wote mkichanganya mawazo na kufanya kazi kwa pamoja,  kazi ya kupelekea umeme wa uhakika wananchi itawezekana.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameitaka Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa, inamaliza changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa vifaa vya umeme ambayo inapelekea wananchi kutopata huduma stahiki katika muda muafaka  na kuwaeleza kuwa mwarobaini wa
changamoto hiyo uko ndani ya TANESCO hivyo walipatie ufumbuzi suala hilo.

Vilevile, ametaka Menejimenti ya TANESCO kuwa na mfumo wa kuwapa motisha watumishi wa Shirika hilo wakiwemo mafundi wa umeme hali hali itakayopelekea watumishi hao kuendelea kujituma zaidi kwenye majukumuyao ya kila siku ikiwemo kuwapa Tuzo wale wanaofanya kazi vizuri zaidi na kuwatambua.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kapinga amechukua fursa hiyo kuwapongeza Wakurugenzi na Mameneja wa TANESCO wa Mikoa na Wilaya kwa kusimamia majukumu yao kwa weledi mkubwa hasa katika kipindi hiki cha mpito ambacho kilikuwa na changamoto ya upatikanaji umeme ambapo hali
sasa inaendelea kuimarika.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbutuka amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa melekezo yake na miongozo ambayo ameeleza kuwa, inazidi kuleta nafuu wa umeme nchini akitaja kuwa maelekezo hayo yamejikita katika maeneo mbalimbali
ikiwemo matengenezo ya miundombinu ya umeme na masuala ya huduma kwa wateja.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Athanasius Nangali alisema kuwa, Shirika hilo lina Kanda Saba, Mikoa 29  na Wilaya 130 za Kitanesco, pia katika mpango wao wa kusogeza huduma karibu na wateja, TANESCO ina viunga 849 ambavyo vinafanya kazi chini
ya Ofisi za Mikoa na Wilaya.

About the author

mzalendo