Featured Kitaifa

TANZANIA YAISIHI MAREKANI KUENDELEZA MCHANGO KATIKA KUTOKOMEZA UKIMWI

Written by mzalendoeditor

Na WAF – Morogoro

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mataifa ya Afrika Kusini na Msumbiji yameisihi Serikali ya Marekani kuidhinisha fedha zitakazochangia katika mwitikio wa UKIMWI kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani katika mwitikio wa UKIMWI (PEPFAR).

Rai hiyo imetolewa tarehe 30 Novemba wakati wa mjadala wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani uliofanyika kwa njia ya mtandao uliowakutanisha wajumbe wa Kongresi ya Marekani, Mratibu Mkuu wa PEPFAR , Dkt John Nkengasong, UNAIDS, Mwakilishi wa Umoja wa Afrika na Mawaziri wa Afya wa Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini.

Kupitia ufadhili wa zaidi ya miaka 20 kutoka PEPFAR kwa nchi zipatazo 50 ambapo takribani dola za kimarekani bilioni mia moja zimetolewa ili kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Afya Mhe Mhe. Ummy Mwalimu emeishukuru PEPFAR kwa kuipatia Tanzania msaada wa dola za kimarekani bilioni 7 kuanzia mwaka 2003 ambazo zimechangia katika kuwaweka kwenye tiba na matunzo zaidi ya watu milioni 1.5 wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo yapatayo milioni 2.2.

“Tunaisihi Kongresi ya Marekani kuidhinisha msaada wa miaka mitano (2024 -2028) ili kufanikisha utokomezwaji wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030” alisisitiza Waziri Ummy.

About the author

mzalendoeditor