Featured Kitaifa

MASOMO YA DINI NI YA KIPEKEE, NI TOFAUTI NA MITAALA YA MASOMO MENGINE

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amebainisha kuwa, elimu inayotolewa kupitia masomo ya dini ni tofauti na ile ya masomo mengine kwani elimu hiyo inahusisha masuala ya imani na hugusa zaidi hisia.

Prof. Mkenda alisema hayo Novemba 30, 2023 katika uzinduzi wa Tanzania Islamic Studies Teaching Association (TISTA) pamoja na makabidhiano ya muhtasari na kitabu cha kwanza cha mwanafunzi cha Elimu ya dini ya Kiislamu, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mfalme Mohamed BAKWATA makao makuu Kinondoni Dar es Salaam.

“Mitaala ya dini ni ya kipekee, ni tofauti na mitaala ya somo la kemia ambayo unaweza kuchukua Wataalamu wa somo hilo ukaangalia na wa nchi nyingine ukaitengeneza, tofauti na ya dini inayovuta hisia na ikatokea tafsiri ambayo si sahihi inaweza kuibuka hisia kali sana”. Amesema Prof. Mkenda.

Aliendelea kusisitiza kuwa, katika hatua za uandaaji wa mitaala tuliona upo umuhimu wa kuwashirikisha katika eneo la imani ili kwa pamoja tusaidiane kuja na mitaala itayokuwa na manufaa kwa wananchi bila kuharibu imani za watu.

Aidha, Prof. Mkenda amemshukuru Mufti wa Tanzania Shekh Abubakar Zuberi na Mufti wa Zanzibar na timu zao kwa ushirikiano anaoendelea kuuonesha katika kufanikisha azma ya mtaala huo wenye manufaa makubwa kwa taifa.

Sambamba na hilo, Prof. Mkenda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kusisitiza uboreshaji wa mitaala mipya utaomsaidia mwanafunzi kujiajiri au kuajiriwa pindi tu atapomaliza elimu.

Nae, Mufti Mkuu wa Tanzania Shekh Abubakar Zubeir amesema, uandaaji wa mtaala huo umeshirikisha umma wa waislamu wote kutoka Tanzania na Zanzibar hivyo kuufanya muhtasari huo kubeba taswira ya michango, mawazo ya waislamu wote nchini.

Vile vile, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania kwa uongozi sahihi ya uliofanyika wa kuweka masomo ya dini katika mtaala huo mpya unaotarajia kuanza kutekelezwa kuanzia Januari 2024.

About the author

mzalendoeditor