Featured Kitaifa

TANZANIA NA SWEDEN ZASAINI MKATABA MSAADA WA TAKRIBAN BILIONI 210 KUIMARISHA KADA YA UALIMU KUPITIA GPE

Written by mzalendoeditor

Na WyEST
Dar es Salaam

Tanzania na Sweden, kupitia Taasisi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kimaendeleo la Sweden (SIDA), zimesaini Mkataba wa msaada wenye thamani ya dola za Marekani milioni 84 sawa na takriban shilingi bilioni 210, kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa Programu ya kuimarisha Kada ya Ualimu nchini.

Mkataba huo umetiwa saini Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El- Maamry Mwamba na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Charlotta Ozaki Marcias.

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema ufadhili huo umekuja katika kipindi muafaka ambapo serikali imeboresha Mitaala ya ualimu hivyo utatumika kama ilivyopangwa kuimarisha utendaji wa walimu kuanzia mwaka 2023/24 hadi 2026/27.

Aidha ameongeza kuwa serikali imetekeleza kwa mafanikio miradi kupitia ufadhili wa awali wa GPE wa dola za Marekani milioni 225 sawa na takriban shilingi bilioni 562 zilizotumika kugharamia utekelezaji wa programu ya kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu awamu ya kwanza kuanzia 2013 – 2018 na awamu ya pili inayoishia 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambae pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkataba huo utaongeza jumla ya misaada kutoka GPE nchini Tanzania kufikia dola za Marekani milioni 309, sawa na takriban shilingi bilioni 773 na kwamba fedha hizo zimekuwa nguvu inayoendesha mabadiliko chanya katika mfumo wa elimu, ukigusa maisha ya wengi.

Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Marcias, alisema kuwa tangu Tanzania ijiunge na Taasisi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (Global Partneship for Education-GPE), mwaka 2013, sekta ya elimu imeboreshwa ikiwemo kupungua kwa msongamano wa wanafunzi wa shule za msingi madarasani kutoka wastani wa wanafunzi 113 hadi kufikia wanafunzi 50.

Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwa wakala wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wa kuboresha mifumo ya elimu nchini ili kuyanufaisha makundi ya walimu kwa kuwajengea ujuzi, maarifa na kuwapa motisha, ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bi. Laura Fringent, aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika maendeleo ya sekta ya elimu na kuahidi kuwa Taasisi yake, itaendelea kutoa mchango wa kuboresha mazingira ya walimu nchini ili kuboresha zaidi elimu kwa faida ya maendeleo ya Taifa.

About the author

mzalendoeditor