Featured Kitaifa

TEWW YALETA NEEMA MPANGO WA ELIMU CHANGAMANI KWA VIJANA  (IPOSA)

Written by mzalendoeditor

 Mwandishi Wetu- Singida

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima  imezindua awamu ya pili ya programu ya  Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya shule (MECHAVI/IPOSA) kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia Taasisi ya KOICA. Mpango huo umezinduliwa leo  mkoani Singida ukilenga kuwakwamua vijana   kielimu na kiuchumi.

Akizundua mpango huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia Taasisi ya KOICA kwa mchango wake katika sekta ya elimu, na hasa kwa udhamini  wa programu ya IPOSA iliyojikita  katika kisomo na elimu ya amali.

“Ni dhahiri kuwa ufadhili huu ni chachu kubwa katika kuinua vijana kielimu hasa kwa kundi hili la vijana walio nje ya shule,” alisisitiza Dkt.  Mganga

Programu ya IPOSA ni fursa muhimu kwa vijana walio nje ya shule kwa kuwa inalenga kupunguza idadi ya vijana walioko mitaani kwa kuwajengea stadi za Maisha, stadi za ujasiriamali,  stadi za kusoma, kuandika na  kuhesabu  na stadi za ufundi wa awali na hatimaye kupata fursa za kujiajiri au kuajiriwa.

Mikoa inayotarajiwa kutekeleza IPOSA kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini  ni Pwani, Tanga, Manyara, Simiyu, Singida na Shinyanga.

Kwa ufadhili huu zitajengwa karakana mpya 30 kwa ajili ya mafunzo, ununuzi wa vifaa vipya vya kufundishia masomo ya ufundi na kufadhili mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wapatao 240. Vile vile takriban walimu 120 watapata mafunzo ya diploma ya elimu ya watu wazima na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Prof. Michael Ng’umbi alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika mikoa 10 ambayo mradi huu  tayari unatekelezwa Tanzania bara. Mikoa hiyo ni  Dodoma, Kigoma, Iringa, Tabora, Mbeya, Dar es Salaam, Njombe, Songwe,Shinyanga na   Rukwa.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Bw. Manshik Shin amesema kuwa mpango huo utaleta manufaa kwa vijana hivyo kuchochea maendeleo.

Aliongeza kuwa serikali ya Korea Kusini imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna wa Elimu Bw. Osca Msalila amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo  katika mikoa 10 ya awali imeiridhisha Serikali ya Korea na hivyo kuridhia kufadhili awamu ya pili.  Ambapo katika awamu ya kwanza program ya IPOSA ilifanikiwa  kudahili vijana 12,000 (Me 5,406, Ke 6,594) kwa programu ya muda mrefu na 30,183 kwa programu ya muda mfupi katika kipindi cha miaka mitatu.

 Kwa kupitia programu hii, ni Dhahiri kuwa changamoto zinazowakabili vijana zikiwemo kutojua kusoma na kuandika na ukosefu  wa ajira zitatatuliwa na programu ya IPOSA.

About the author

mzalendoeditor