Featured Kitaifa

SERIKALI KUWANOA WANAMIPANGO

Written by mzalendoeditor

Na Georgina Misama – MAELEZO

Serikali kupitia Tume ya Mipango imekutana na wanamipango kutoka kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma na Halmashauri nchini ili kupata mwelekeo wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu katika sehemu zao za kazi.

Akiongea mapema leo Novemba 28, 2023 Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Lawrence Mafuru amesema kuwa kongamano hilo pamoja na kuwapa Wanamipango nafasi ya kufahamia lakini lina lengo la kuwanoa kwa mada mbalimbali zitakazowasilishwa ili kuendana na matarajio ya Serkali.

“Serikali inatekeleza majukumu yake kwa kupanga na kila jambo linaanzia kwenye Idara ya Mipango, tunashukuru tumeweza kuwaleta pamoja wanamipango wote wa Serikali, hapa tutapata nafasi ya kufanya tathimini ya changamoto tulizonazo na kwa kuwa sisi ni wapangaji tuanze pia kutafuta majawabu ya changamoto hizo,”alisema Mafuru.

Alisema kutokana na kuundwa kwa Tume ya Mipango na matakwa ya kisheria kwamba Tume hiyo itakuwa mratibu na msimamizi mkuu wa kada hiyo ya wanamipangoTume imeona huu ni wasaa mzuri kuwakumbusha majukumu yao Wanamipango hao katika zama mpya za upangaji maendeleo.

Leo ni siku ya pili ya Wiki ya Wanamipango 2023 ambapo wanapango zaidi ya 400 wamehudhuria kongamano hilo linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo linaongozwa na kaulimbiu ‘Fikra za Pamoja na Utekelezaji Uliratibiwa kwa Ustawi Jumuishi’.

About the author

mzalendoeditor