Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU ATAKA RIPOTI MAALUM YA CAG MBOZI IFANYIWE KAZI HARAKA

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi kwenye Uwanja wa Malori Vwawa Wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe,

….

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo wawasake watu 72 waliohusika na upotevu wa fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ili wazirudishe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

“RC na KU yako pitieni ripoti ya ukaguzi maalum uliofanywa na CAG kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha hapa Mbozi na muwashirikishe madiwani. Watu hao watafutwe walipe hela zetu na wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Novemba 24, 2023), wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Mbozi, Madiwani kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Akizungumzia mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu alisisitiza suala la uaminifu miongoni mwa watumishi wa umma hasa wa vitengo vya manunuzi na uhasibu ambapo alisema taarifa hiyo imebainisha uwepo wa wizi wa wazi katika manunuzi.

“Mojawapo ya masuala yaliyojitokeza kwenye taarifa hiyo ni manunuzi ya vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 406 bila risiti. Haiwezekani kabisa kwamba sisi tukaenda kufanya manunuzi lakini hatudai risiti wakati tunajua ni hela ya Serikali.”

Akizungumzia tuhuma za ujenzi wa shule ya sekondari ya Kisimani, watumishi hao walibadilisha ramani bila idhini kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusababisha gharama za ujenzi zipande. “Tulikuwa na ramani ya awali kwa gharama ya sh. milioni 466 lakini ninyi mkabadilisha ramani na kuongeza sh. milioni 206 lakini timu ilipoenda kukagua eneo la mradi, ilibaini uwepo wa nyufa, fremu za milango kupinda na kupishana na venti 28 kutowekewa nondo wala vioo.”

Akibainisha makosa mengine, Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo imeonesha kuwa kuna upotevu wa sh. 292,375,419.93 za makusanyo yaliyoainishwa katika Mfumo wa Mapato (LGRCIS) lakini hazikuwasilishwa benki.

“Kati ya hizo, shilingi 90,670,578.14 zilikusanywa lakini hazikuwasilishwa benki na wakusanyaji 44; shilingi 66,821,913.26 zilikuwa ni miamala iliyoingizwa kimakosa katika mfumo huo; shilingi 65,570,298.61 kutofafanuliwa kutokana na wakusanyaji 28 ambao ni mawakala na Watendaji wa Vijiji kutowasilisha ufafanuzi; shilingi 64,182,729.91 ziliwasilishwa benki na wahusika wakati ukaguzi maalum unaendelea na shilingi 5,129,900 ziliwasilishwa katika akaunti ya amana ya Halmashauri badala ya akaunti  ya mapato.”

Akitoa mifano zaidi, Waziri Mkuu alisema: “Kuna wakala alikusanya sh.15,310,500.00 lakini yeye akapeleka benki sh. 310,500.00 tu na ile sh. milioni 15 ameweka mfukoni, haikubaliki. Mwingine alikusanya 2,357,100.00 akapeleka benki sh. 875,300.00 na sh. milioni 1.481,800.00 amekula. Wa tatu alikusanya sh. 12,597,020.00 akapeleka benki sh. 101,500.00, na wa nne alikusanya sh.18,902,710.00 akapeleka benki sh. 13,725,510.00 na pesa ilibakia ya sh.5,177,200 ameila. Hawa mnawajua na baadhi yao ni watendaji wa vijiji. Watafutwe na warudishe hizi fedha.”

Alisema upotevu mwingine wa fedha ulitokana na mauzo ya kahawa za wakulima ambapo mzigo wa kahawa wenye thamani ya sh. bilioni 1.18 umepotea. “Halmashauri hii inafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Kahawa. Kahawa za wakulima zilipotea lakini pia mlishindwa kusimamia ushuru wa zaidi ya sh. milioni 75 ambao ulipaswa kulipwa na bodi hiyo na kuingia Halmashauri.”

Aliwasisitiza watumishi hao watambue kuwa kazi ya makusanyo ya mapato inahitaji uaminifu na uadilifu. “Wakati Serikali inakimbizana kukusanya mapato, wako watu wengine wanatushika mashati na kutuvuta tusiende mbele.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi kwenye Uwanja wa Malori Vwawa Wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe, Novemba 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

About the author

mzalendo