Featured Kitaifa

JAJI MOHAMED CHANDE AMEWATAKA WAHITIMU KUTUMIA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA KUWA FURSA.

Written by mzalendoeditor

 

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mohamed Chande Othman amewataka Wahitimu kutambua kuwa maisha Kitaaluma ni mitazamo ya maisha yanayobadilika kila wakati kutokana na Misukumo ya Teknolojia na Mazingira.

Ameyasema hayo kwenye mahafali ya 42 ya Chuo hicho yaliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Joseph Sinde Warioba ambapo amesema Wahitimu wanatakiwa kutumia mabadiliko hayo kama fursa ili kuleta maendeleo.

“Kwa wale wanafunzi ambao hawajahitimu lakini wanazo ndoto za kuhitimu nawaasa kusoma kwa bidii ili watakapohitimu wawe na weredi wa kutosha katika fani zao kwasababu nisingependa kuona wahitimu wa Chuo hiki chenye historia na uzoefu wa muda mrefu katika kufundisha masomo ya Fani za Kilimo wawe wasiojiamini katika kazi zao za kuhudumia watanzania”, alisema Jaji Mohamed Chande.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema Chuo kimekuwa kikifanya Mafunzo katika Kampasi zote tatu, Edward Moringe, Solomon Mahlangu na Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema Chuo kimeendesha program mbalimbali za masomo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Kampasi zake zote tatu ikiwemo Astashahada, Stashahada, Shahada za Awali, Stashahada za Uzamili, Shahada za Umahiri na Shahada za Uzamivu.

Katika Mahafali ya 42 Wahitimu 3095 kutoka programu 74 wametunukiwa vyeti ambapo wanawake ni asilimia 43.9 ya Wahitimu wote huku wakihudhurishwa kwa mara ya kwanza Wahitimu wa kwanza wa Ngazi ya Shahada kutoka Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi.

Pia wahitimu 2,811 ni kutoka Shahada za Awali ambapo wanaume ni 1,574 na wanawake 1,237, Shahada za Umahiri wahitimu 56 wanaume 29, na wanawake 27, Stashahada ya Juu ya Elimu wahitimu 2 wote wakiwa ni wanaume, Shahada za Uzamivu 18, wanaume 10 na mwanamke 8, wahitimu wa Stashahada 140, wanaume 73 na wanawake 67 vilevile wahitimu 68 wa Astashahada , wanaume 47 na wanawake 21.

About the author

mzalendoeditor