Featured Kitaifa

MAKONDA:CCM INATAKA KUONA MGOGORO WA GGM NA VITONGOJI VYA GEITA UNATATULIWA NA WANACHI WA GEITA WANAFAIKE NA NADINI KATIKA ARDHI YAO 

Written by mzalendo

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Cde. Paul Makonda amemuagiza Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ikiwa ni agizo la Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha Mgogoro wa mipaka ya ardhi baina ya Mgodi unaomilikiwa na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na Vitongoji vya Geita unatatuliwa kabisa.

Mwenezi Makonda amesema Mgogoro huo umekuwa kero kubwa kwa Wananchi hao kwani umedumu kwa zaidi ya miaka 20 ambapo amemuelekeza Waziri Mavunde siku ya kesho tarehe 12 Novemba, 2023 kufika Mkoani Geita kushughulikia suala hilo.

Akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara na Wananchi wa eneo hilo, Mwenezi Makonda mara baada ya kupokea kero hiyo alimpigia simu Waziri wa Madini kujua Serikali ina mpango gani kutatua hadha hiyo.

Naye Waziri Mavunde alijibu kwa kusema kuwa tayari yupo Mkoani Geita na kesho atakuwa na Kikao kinachohusiana na utatuzi wa mgogoro huo ambapo amemueleza Mwenezi Makonda kuwa alishafika Geita kwa suala hilo na walikaa kikao na aliahidi baada ya mwezi mmoja atarudi ilikusudi kumaliza kabisa mgogoro huo.

Mwenezi Makonda amesema “Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ,imeboresha kwa kasi sekta ya Madini kiasi kwamba hadi wachimbaji wadogo wanapewa vibali vya kufanya shughuli hiyo ya uchimbaji madini hivyo kwa namna yoyote ile Chama kinataka kuona mgogori huo unafikiwa mwisho”

Ameyasema hayo leo tarehe 11 Novemba, 2023 wakati alipozungumza na Wananchi wa Wilaya ya Geita akiwa ziarani kikazi katika Mkoa wa Geita

About the author

mzalendo