Featured Kitaifa

HAKIKISHENI WATOTO WACHANGA HAWAPATI SHIDA WATUMIAPO KADI ZA WAZAZI WAO.

Written by mzalendo

Na WAF – DODOMA

Naibu Waziri wa Afya, Dkt.Godwin Mollel amewataka watendaji wa mfuko wa bima ya afya na vituo vyote vya huduma za afya nchini kuhakikisha watoto na wazazi hawapati shida iwapo mama atakuwa na kadi yake inayoonyesha ushahidi wote kuhusu mtoto husika na ni mtoto wangapi kwenye familia.

Dkt. Mollel ametoa agizo hilo leo Jijini Dodoma katika Mkutano wa Bunge wa 13 Kikao cha Nne wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, swali Namba. 61 kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe.Martha Nehemia Gwau aliyeuliza Je, Serikali haioni kuna haja ya Watoto wachanga kutumia Bima za Afya za Mama zao

Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ilishatoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha Watoto wachanga wenye uhitaji wa huduma wanapata huduma za afya bila kikwazo chochote.

Vile vile Dkt. Mollel ameongeza kuwa kuwa watoto wanaozaliwa katika hospitali na vituo vya kutolea Huduma za afya nchini ambao wazazi wao wana Bima za afya watibiwe kwa kutumia bima za wazazi wao.

Niwaase wazazi na viongozi wa hospitali husika kukomesha kabisa matukio ya kughushi nyaraka ambazo pia ndio zinapelekea kuwepo kwa usumbufu wakati mwingine”, ametoa wito Dkt. Mollel.

About the author

mzalendo