Featured Kitaifa

WAZIRI SILAA ACHARUKA ASIMAMISHA WATUMISHI 9 ARDHI KUPISHA UCHUNGUZI

Written by mzalendo

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 23,2023 jijini Dodoma.

Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasimamisha kazi watumishi tisa waliokuwa wakifanya kazi katika halmashauri ya Jiji la Dodoma na wawili halmashauri ya Jiji la Mwanza kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 23,2023 Jijini Dodoma na  Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo.

Waziri Sllaa amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kutoa maelekezo mbalimbali Oktoba 3,2023 yaliyolenga kuboresha huduma za sekta ya ardhi katika halmashauri hizo mbili za Dodoma na Mwanza.

“Wizara yangu itaendelea kuchukua hatua kwa watumishi wa sekta ya ardhi watakaokiuka maadili ya utendaji kazi lakini pia tayari TAKUKURU imefahamishwa kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watumishi waliosimamishwa kazi na utekelezaji unaendelea,”amesema Sllaa.

Aidha amemuagiza mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuwaondoa watumishi 25 waliokuwa wamesalia kwakujitolea ambapo awali walikuwa 106 baada ya wengine kuondolewa April 25 mwaka huu.

Amesema kuwa wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali kwa kushirikiana na mamlaka hatua itakayo wawezesha kuboresha utaendaji kazi katika sekta ya ardhi nchini.

About the author

mzalendo