Featured Michezo

RC MOROGORO AWATAKA WAFANYAKAZI TPA KUTUMIA MICHEZO YA BANDARI 2023 KUIMARISHA AFYA ZAO

Written by mzalendo


Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe.Adam Malima  amewataka wafanyakazi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania-TPA kutumia michezo ya bandari 2023 kuimarisha afya zao na kuongeza tija na ufanisi mahala pakazi.

Katika hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe.Rebeca Nsemwa   wakati wa ufunguzi wa michezo ya bandari, tarehe 23 Oktoba, 2023 mjini Morogoro, amesema ni muhimu kwa Watumishi hao kuendelea kushirikiana ili kuikuza sekta ya michezo ndani ya mamlaka hiyo.

“Tuitumie michezo hii kama sehemu ya kampeni ya kutaka kuimarisha afya zetu lakini kubwa zaidi kutaka kuongeza tija na ufanisi kazini na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali,” amesema Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Juma Kijavara ametoa Rai kwa Watumishi hao kuwa na nidhamu wakati wote wa michezo hii na kuitumia vema kujenga mahusiano mema na urafiki wenye tija ili kutekeleza vyema majukumu yao kazini.

“ Naomba nitoe wito na kuwasisitiza Wanamichezo wote kushiriki michezo hii kwa nidhamu ya hali ya juu na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma,” amesema Mhandisi Kijavara.

Katika siku ya kwanza ya michezo hii timu ya bandari ya Dar-es-salaam imetoa onyo kali kwa timu nyingine baada ya kuwanyuka timu ya bandari Mtwara kwa mabao 6-0, Bandari Tanga wakipata ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya Timu ya makao makuu ya TPA, huku Bingwa mtetezi Timu ya Terminal II wakianza vema Kampeni yao ya kutetea ubingwa kwa kupata ushindi wa mabao Matatu kwa bila dhidi ya Shirika la Bandari Zanzibar.

katika matokeo mengine Bingwa mtetezi wa mpira wa netiboli timu ya Bandari Dar-es-salaam wamewatambia Bandari ya Tanga mabao 45-23 huku Makao makuu wakiwakandika Kampuni ya huduma za Meli ( MSCL) magoli 78 kwa 1.

Kwenye mchezo wa kuvutana kwa Kamba, ubabe umeendelezwa na Timu za Wanaume na Wanawake za Makao makuu sawa na utemi wanaouendeleza Timu ya Bandari ya Tanga kwa Wanaume na Bandari ya Dar es Salaam kwa Wanawake.

Michezo hii ya siku nane inafanyika katika viwanja vya Jamhuri na Chuo Kikuu cha Kiislamu Mjini Morogoro ikishirikisha Wanamichezo takribani 800 kutoka timu Nane za TPA Makao Makuu, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga, Bandari Mtwara, Bandari za Maziwa, Shirika la Bandari Zanzibar-ZPC, Kampuni ya huduma za Meli – MSCL na Timu ya Terminal II ( Zamani ikiitwa TICTS).

 

About the author

mzalendo