Featured Kitaifa

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA USTAWI WA WAFANYAKAZI

Written by mzalendoeditor

 

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe Mhe. Fatuma Toufiq akieleza jambo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bungeni leo Oktoba 18, 2023, Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) leo Oktoba 18, 2023 Bungeni, Jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akichangia jambo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Bungeni, Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja akieleza jambo wakati wa kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 18, 2023 Bungeni Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imepongezwa kwa kuendelea kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wanaopata madhira kazini kwa kuwalipa fidia zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe.Fatuma Toufiq ametoa kauli hiyo Oktoba 18, 2023 jijini Dodoma kwenye kikao cha kamati hiyo na menejimenti ya WCF cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo, mafanikio na mikakati ya kukabiliana na changamoto.

“Serikali inafanya kazi nzuri sana, tunatambua juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi kwa madhara wanayoyapata kazini, kamati inalitambua hilo na tutaendelea kuishauri serikali ikiwezekana bajeti iongezeke na kuimarisha zaidi ustawi wa wafanyakazi ili wanaoumia kazini wapate stahiki zao. Tunasisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu mfuko huu,”amesema.

Naye, Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameihakikishia kamati kuwa WCF itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kupata huduma zinazostahili wanapopata madhira yeyote wakiwa kazini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas Katambi, amesema kwa mujibu wa sheria kila taasisi ambayo inaajiri inapaswa kujisajili WCF na lengo la mfuko ni kusajili wanachama 3,000 kwa mwaka.

Aidha, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja,ameiahidi kamati kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuisimamia WCF kuzingatia ushauri na maoni ya kamati hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema kwa mwaka 2022/23 madai 4,306 yalichakatwa na kutoa mafao yenye thamani ya Sh.Bilioni 17.9 na imechangiwa na kuongezeka kwa uelewa kwa jamii.

About the author

mzalendoeditor