Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YASHAURI MIKOPO YA ASILIMIA 10 ISIMAMIWE NA BODI YA MIKOPO YA SERIKALI ZA MITAA

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeitaka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha inatoa nafasi kwa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kusimamia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu ili ziweze kutumika na kuwafikia walengwa ipasavyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Denis Londo ameyasema hayo Oktoba 17, 2023 kwenye kikao cha kamati hiyo cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za bodi hiyo sambamba pia na upokeaji wa taarifa ya utekelezaji ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT).

Mhe. Londo amesema ni vema Bodi hiyo ikahusishwa pindi mikopo hiyo inapotolewa ili kuweza kuzisimamia taasisi za kibenki ambazo ndizo zimepewa jukumu la kutoa mikopo hiyo.

“Agizo la Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan lilikua wazi kabisa kuwa hivi sasa zile 10% za vijana, wanawake na walemavu zitapitishiwa kwenye taasisi za fedha. Sasa ni vema TAMISEMI ikawapa rungu Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kusimamia mchakato huu kwa sababu sisi kamati hatutoweza kuziita taasisi hizo hivyo bodi hii iwe kama mkono wa serikali katika kusimamia fedha hizo,” amesema Mhe. Londo.

Mhe. Londo ameitaka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuandaa semina itakayowawezesha wajumbe wa kamati hiyo kuweza kuzifahamu taasisi ambazo ziko chini ya ofisi hiyo ili kuwajengea uelewa wa pamoja lengo likiwa kurahisisha utendaji kazi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi ameihakikishia kamati hiyo kuwa watafanyia kazi mapendekezo na maelekezo yao huku pia akizitaka taasisi hizo Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa na ALAT kuandaa semina zitakayowawezesha wajumbe wa kamati kufahamu majukumu yao na kujenga uelewa wa pamoja.

About the author

mzalendoeditor