Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kwa mara nyingine kwa mafaniko makubwa kwa kushirikiana na Korea International Foundational for Health Care na Africa Future Foundation imefanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanne ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi.
Upandikizaji huo ni wa kipekee hapa nchini kwa kuwa umetumia utaalamu wa kisasa Duniani ambapo figo imevunwa kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia njia ya matundu madogo (Hand assisted Laparoscopic Donor Nephrectomy).
Akizungumzia upandikizaji huo katika hafla ya kuwaaga waliopandikizwa figo, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema utaalamu uliotumika kuvuna figo kwa kutumia matundu unafanyika Mloganzila pekee kwa Hospitali za Umma nchini na Afrika Mashariki na Kati.
“Kwa kutumia njia ya matundu mchangiaji anakuwa na kovu dogo, anakaa hospitali kwa muda mfupi takribaini siku mbili hadi tatu kitu ambacho kinasaidia kupunguza gharama kwa hospitali na mchangiaji pia” amebainisha Prof. Janabi.
Aidha, Prof. Janabi ameishukuru Serikali kwa uwekezaji ilioufanya ambapo amefafanua kuwa Mloganzila kuna vyumba vya upasuaji vya kisasa na vyumba vya uangalizi maalumu vyenye mashine na vifaa vya kisasa na pia kuna wataalamu bingwa na bobezi waliojengewa uwezo na Serikali katika nyanja tofauti tofauti.
Kwa upande wake Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Dkt. Kim Sun Pyo amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Mloganzila katika kuwajengea uwezo wataalamu, na kufanikisha huduma za kibingwa hapa nchini kwa lengo la kuendelea kuboresha afya za Watanzania.
Naye, Mtaalamu Mwelekezi kutoka Korea Kusini, Prof. Park Kwan Tae amesema ataendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mloganzila ambapo ameongeza kuwa huduma za upandikizaji kwa njia ya matundu zitafanyika mara kwa mara na hatimaye hospitali hii kuwa kinara katika upandikizaji kwa kutumia njia ya matundu Afrika.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Antony Gyunda ameishauri jamii kuwasaidia ndugu zao wenye changamoto ya maradhi ya figo kwa kuwa mtu akichangia figo hawezi kupata changamoto zozote za kiafya.