Featured Kitaifa

MARIAM ULEGA AWAKINGIA KIFUA WATOTO WA KIKE WASIBAGULIWE

Written by mzalendoeditor
Na Victor Masangu,Kibaha
 
Wazazi na walezi wametakiwa kuachana na vitendo vya kuwabagua watoto wa kike na kuwafanyia ukatili wa kijinsia na badala yake wanapaswa kubadilika na kuwapatia haki zao za msingi ikiwemo suala la kuwapatia elimu iliyo bora ili kutimiza ndoto zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake Mkoa wa Pwani Bi.Mariam Ulega wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike  duniani ambayo yamefanyika katika shule ya sekondari Bundikani iliiyopo Wilayani Kibaha mkoani Pwani ambayo yameandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Room to Read linalojishughulisha na elimu kwa msichana.
Mwenyekiti huyo ambaye pia  mke wa Waziri wa mifugo na uvuvi  Abdalah Ulega ndiye alikuwa  mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambapo pia aliwapa motisha wanafunzi kwa kununua vitu mbali mbali ambavyo wamevitengeza kutokana na ujuzi walionao ikiwemo sabuni.
Alisema kwamba anatambua kwa sasa bado kuna changamoto nyingi ambazo zinawakabili watoto wa kike ambazo zinapelekea kukwamisha ustawi na maendeleo yao kutoka na kufanyiwa mambo ya ubaguzi na mambo mengine ya ukatili wa kijinsia pamoja na kupata mimba za utotoni.
Kwa upande wake Meneja miradi wa elimu kwa msichana na usawa wa Kijinsia Hadijs Hassan alisema kwamba lengo la shirika lao la Room to Read ni kuweka mipango ya kuimarisha usawa wa Kijinsia katika kutoa elimu ya stadi za usomoji ikiwa pamoja na kujenga tabia ya usomaji.
Pia alibainisha kwamba mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na serikali,mashirika washirika na jamii zilizopo katika maeneo ya mradi huo ambapo shirika hilo hadi sasa linafanya kazi katika nchi 23 ikiwemo Tanzania 
Kadhalika katika hatua nyingine  Mwenyekiti ametoa Rai kwa serikali ya Mkoa wa Pwani pamoja na wadau wengine wa elimu  kuendelea kuandaa mpango endelevu wa kufundisha elimu ya stadi za maisha hususani kwa watoto wa kike hata baada ya kumalizika kwa  utekelezaji wa mradi wa elimu kwa msichana na usawa wa kijinsia.
Naye Afisa elimu wa Mkoa wa Pwani Sara Mlaki alibainisha kuwa wao kama serikali wanaunga mkono jitihada ambazo zinafanywa na Shirika hilo la Room to Read na kwamba watakuwa nao bega kwa bega katika kuona mradi huo unatekelezwa bila vikwazo vyovyote.
Pai aliongeza kuwa kwamba mradi huo umeweza kuleta matokeo chanya kutokana na kuwapatia walimu mafunzo  mbali mbali kwa ajili ya uwezeshaji wa stadi za maisha kwa wanafunzi,na utekelezaji wake umeanza tangu mwaka 2022,kwa walimu 22 kutoka halmashauri ya Chalinze kunufaika.
Mwaka huu wa 2023 shirika la Room to Read limeungana na wadau mbali mbali duniani kuachimishs siku ya mtoto wa kike duniani ambapo kauli yake inasema “Wekeza katika elimu kwa msichana na stadi za maisha kwa maendeleo endelevu.

About the author

mzalendoeditor