Featured Kitaifa

MKE WA PROF. JAY AIBUKA NA KIJIJI CHA NGURUWE DODOMA

Written by mzalendoeditor
Mkurugenzi wa PigInvest International Plc Bi. Grace Mgonjo ambaye pia ni Mke wa Msanii na Mwanasiasa Maarufu ndani nje ya nchi ya Tanzania Joseph Leonard Haule ‘Professor JAY’ Mwana wa Mituringa ametambulisha mradi wa ufugaji wa Nguruwe almaarufu Kitimoto katika kijiji cha Zamahero Mayamaya wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Oktoba 3,2023, Bi. Mgonjo amesema yeye na mmewe Prof. JAY wameamua kuja na mradi huo kwa Umma baada ya kuona nyama ya nguruwe almaarufu Kitimoto inaliwa sana na Watanzania.
 
“Tumeamua kuja na mradi huu wa Kijiji cha Nguruwe ukizingatia kuwa nyama hii inatumiwa na watanzania takribani Milioni 48 na katika Afrika inatumiwa na watu takribani Bilioni 1.4 hii ni takribani asilimia 70 ya watu wote”,ameeleza.
Amefafanua kuwa mtu akiwekeza kwenye Nguruwe mmoja anaweza kupata mpaka mara mbili ya uwekezaji wake ndani ya mwaka mmoja.
Ameongeza kuwa uwepo wa chakula kingi cha nguruwe hususani mashudu ya Alizeti katika mikoa ya Kanda ya Kati imekuwa kichocheo kikubwa cha kuanzisha mradi wa ufugaji wa Nguruwe Mkoani Dodoma katika kijiji cha Zamahero Mayamaya wilaya ya Bahi.
“Ujue miaka mingi watanzania wamekuwa wakifuga nguruwe kienyeji bila kurasimisha shughuli za ufugaji na hivyo serikali inakosa mapato makubwa kwenye mifugo inayopendwa kuliko yote, hivyo tunaamini mradi huu utakuwa na manufaa makubwa katika taifa”,amesema Mgonjo.
Aidha ameiomba Serikali iwasaidie kuutangaza mradi huu ambao unaajiri wanawake wenye maisha magumu zaidi ya 200 na tayari wengine wako shambani wakitayarisha shamba la Nguruwe.
Gharama za mradi:
Mradi huo wa ufugaji nguruwe utagharimu zaidi ya Bilioni 270 mpaka kuisha kwake 2026.
“Magari ya Friji zaidi ya 100 yatakuwepo eneo la mradi (site) kwa ajili ya kusambaza nyama Tanzania nzima na duniani kwa ujumla. Tutauza Hisa ili kukuza mtaji na pia tutawaalika wananchi kuwekeza katika mradi huu mkubwa, hii ni fursa kubwa hasa kwa watu wa maofisini na walio busy”,ameeleza.
Amesema Kiwanda cha kuchakata nyama ya nguruwe kitatengenezwa hapo hapo Zamahero Mayamaya Bahi mkoani Dodoma Tanzania ambapo idadi ya Nguruwe ni Milioni 3.
“Endapo kuna mtu anahitaji maelezo zaidi awasiliane naye kwa simu namba 0627122122 au 0627188188″,amesema
 
Katika hatua nyingine Mke wa proffessor Jay ameiomba Serikali pia iangazie mradi wa Kijiji cha Vanilla kwani serikali itapata fedha nyingi sana za kodi na fedha za kigeni kupitia mradi huo.

About the author

mzalendoeditor