Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Jubilee ya Miaka 125 ya uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea Mkoani Songea lililofanyika Peramiho, Oktoba 1, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga. Kulia ni Mkewe Mama Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu Sh. Milioni 10 kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji katika Jimbo Kuu la Songea, Oktoba 1, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Songea, Askofu Mkuu Damian Dallu baada kushiriki katika ibada ya Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji kwenye Jimbo Kuu Katoliki la Songea. Jubilei hiyo ilifanyika kwenye kilima cha Peramiho Mkoani Songea, Oktoba 1, 2023. Kulia ni Mkewe Mama Mary Majaliwa na kushoto ni Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Askofu Bruno Ngonyani. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu wa Kanisa Katoliki walioshiriki katika Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji kwenye Jimbo Kuu la Songea. Jubilei hiyo ilifanyika kwenye kilima cha Peramiho mkoani Ruvuma, Oktoba 1, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa staha, weledi na uadilifu ili kuzitumia rasilimali zilizopo nchini kujiletea maendeleo.
“Nchi yetu imebarikiwa fursa nyingi za kiuchumi, ili jamii ione matunda ya uwepo wa fursa hizo tunategemea sana nguvu kazi ya vijana katika kuzitumia rasilimali zilizopo”
Ametoa wito huo leo Jumapili (Oktoba 01, 2023) wakati wa Jubilei ya miaka 125 ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, kwenye kilima cha Peramiho, Songea mkoani Ruvuma.
Aidha, amezisihi Taasisi za dini kuweka mipango mahsusi na shirikishi ya malezi ya vijana. “Tumieni nafasi zenu kuongeza msukumo wa malezi kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwafuatilia kwa karibu na kuhimiza ushiriki wao kwenye vyama vya kitume”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa masuala ya kipaumbele yanayohusu ustawi wa Taifa.
“Niwasihi sana mtuunge mkono kuhamasisha uhifadhi wa mzingira na matumizi ya nishati safi, kampeni za kupanda miti na usafi wa mazingira, kukemea vikali vitendo vya mmomonyoko wa maadili, matumizi ya madawa ya kulevya na kukemea vitendo vya rushwa”
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyapongeza madhehebu ya dini kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye sekta za elimu, afya, maji na huduma nyingine za kijamii hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Kazi hiyo mnayoifanya ya kutoa huduma kwa jamii ni kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kusogeza huduma zote muhimu karibu na wananchi”
Katika Jubilei hiyo, Rais Dkt. Samia ametoa shilingi milioni kumi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 125 ya jubilei ya Uinjilishaji katika jimbo kuu Katoliki la Songea.
Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Damian Dallu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli mbalimbali za huduma za jamii na uinjilishaji zinazofanywa na kanisa katoliki nchini.