Featured Kitaifa

SHULE MPYA YA MRADI WA BOOST WAONDOA KERO ZA WANANCHI KATA YA KIBIRIZI-KIGOMA

Written by mzalendoeditor

Na. Asila Twaha, Kigoma MC

Wananchi wa Kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Mkoani Kigoma wamesema kukamilika kwa shule Mpya ya Msingi Kiheba iliopo Mtaa wa Bushabani, Kata ya Kibirizi, Tarafa Kigoma Kaskazini Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji inayojengwa kupitia Mradi wa BOOST itasaidia kuondoa kero kubwa za ukosefu wa shule ya msingi kwa muda mrefu kwa wanafunzi na wananchi wanaoishi eneo hilo.

Hayo yameonekana Septemba 20, 2023 wakati wa ziara ya pamoja ya timu ya wataalam Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Wataalam wa Benki ya Dunia lengo likiwa ni kukagua utekelezaji wa Miradi ya Elimu katika Mkoa wa Kigoma katika Halmashauri ya Kigoma Manispaa, Uvinza na Kigoma Ujiji inayotekelezwa kwa Mradi wa BOOST na SEQUIP.

Diwani wa Kata ya Kibirizi Mhe. Ramadhan Ruhuso akizungumza kwa niaba ya wananchi amesema, ujenzi wa shule hiyo hadi sasa upande wa madarasa umefika 90% Jengo la Utawala 95%, Madarasa ya elimu ya Awali 85% na Vyoo 80% ambapo maendeleo yake ni mazuri na kukamilika kwa kwake utasaidia kuondoa adha kwa wanachi wa eneo hilo.

Amesema kufikia kwa hatua nzuri ya ujenzi ni ushirikiano kati ya jamii na viongozi kamati ya shule, viongozi wa Serikali za kata, mitaa na wataalamu Ofisi ya Mkurugenzi ameshauri Serikali iendelee kushirikiana na jamii kutekeleza miradi ili ifanikiwe kukamilika kwa haraka.

Kwa upande wa Mratibu Msaidizi Mradi wa BOOST Ofisi ya Rais – TAMISEMI Reuben Swilla ametoa wito kwa uongozi wa shule wanakamilisha taratibu za ukamilishaji wa shule hiyo kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni kama ilivyoelekezwa na hakuna sababu ya kutokamilisha sababu fedha zote zilishatolewa.

Swilla ametoa wito kwa viongozi wa shule hiyo kukamilisha ujenzi kulingana na miongozo inavyotaka lakini pia kukamilika kwa ujenzi kuongeze fursa ya utoaji wa elimu ya msingi katika Manispaa ya Kigoma. Jamii ihakikishe inatoa mahitaji muhimu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na chakula.

Awali taarifa iliyosomwa na Mwalimu Mkuu Andrew Matanwa imesema shule hiyo ilipokea milioni 561 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya yenye mikondo miwili madarasa 14 elimu msingi, jengo la utawala, madarasa 2 elimu ya awali yenye matundu 6 ya choo, matundu 16 ya choo elimu ya msingi, matundu 2 ya choo cha walimu na kichomea taka ngumu.

Amesema kukamilika kwa shule hiyo itapunguza msongamano wa watoto madarasani 50% sababu wanafunzi zaidi ya 800 watahamia katika shule hiyo, itapunguza utoro wa wanafunzi 90%,itaongeza ari na hamasa ya wanafunzi kupenda shule hivyo kuongeza ufaulu wa mitihani na pia utapunguza ukatili kwa watoto mimba za utotoni kwa kutotembea umbali mrefu kwenda shule.

Naye Fundi Ujenzi Bi. Zainab Mohamed ameishukuru Serikali kwa kujenga shule hiyo hapo amesema, mbali ya kupata kazi ya kibarua ambapo analipwa kumsaidia kuendesha familia yake lakini pia amesema, uwepo wa shule hiyo itasaidia kupunguza adha waliokua wanaipata kama wazazi sababu uwepo wa ukaribu wa shule itasaidia kuweza kufuatilia maendeleo ya mtoto na imepunguza changamoto ya shule ya awali hasa wakati kipindi cha masika kunakuwa na changamoto sababu ya mto uliopo mvua zikinyesha watoto wanashindwa kufika shule.

About the author

mzalendoeditor