Featured Kitaifa

KOICA YAONESHA NIA YA KUSAIDIA MFUKO WA AFYA ZANZIBAR

Written by mzalendoeditor
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akizungumza wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) kwa nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, Seoul, Korea Kusini. 
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) kwa nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, akizungumza wakati wa kikao na Ujumbe kutoka Tanzania kilichofanyika katika Ofisi za Shirika hilo mjini Seoul, Korea Kusini. 
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Aboud Hassan Mwinyi, akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) kwa nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, wakati wa kikao cha ujumbe wa Tanzania na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) kwa nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, Mjini Seoul, Korea Kusini. 
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Seoul, Korea Kusini)
Na. Saidina Msangi, WF, Seoul Korea Kusini
 
Tanzania pamoja na mambo mengine imeliomba Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) kusaidia Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) wa Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi kwa mwaka 2024/2025. 
 
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa KOICA anayesimamia nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, Seoul, Korea Kusini. 
 
Alisema kuwa lengo la kuboresha Mfuko wa Afya wa Pamoja Zanzibar ni kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na kwa gharama nafuu kwa wananchi hususani, kujenga mfumo mzuri wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya Afya ngazi za chini.
 
“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2023 Mfuko wa Afya wa Pamoja Zanzibar ulichangia jumla ya dola za Marekani milioni 7.1 sawa na shilingi takribani bilioni 16.3 kwenye sekta ya afya ambapo kiasi kikubwa cha fedha hizo kilielekezwa kwenye ngazi ya Wilaya’’alieleza, Bi. Amina Khamis Shaaban. 
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KOICA anayesimamia nchi za Afrika Mashariki, Bw. Chon Gyong-shik, alisema kuwa atafanya jitihada za kuangalia namna ya kuwezesha ombi la Zanzibar kupatiwa msaada ulioombwa na pande mbili zitashirikiana kufanyia kazi suala hili. 
 
Alieleza kuwa wasilisho la mradi likipokelewa na Shirika hilo hufanyiwa kazi ndani ya miaka miwili kufikia utekelezaji hivyo kama mradi ukipitishwa mwaka huu ni hadi mwaka 2026 na kuahidi kuwa mara baada ya kupokelewa kwa wasilisho pande zote mbili zitaona namna ya kufanya ili kupunguza muda wa uchambuzi ili mradi huo utekelezwe kuanzia mwaka 2025. 

About the author

mzalendoeditor