Featured Kitaifa

AFISA FEKI WA NIDA AKAMATWA 

Written by mzalendoeditor

Na Calvin Minja-NIDA

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanzisha operesheni maalum ya kuwasaka na kushughulikia watu wanao walaghai  wananchi kuwa ni watumishi wa NIDA kwa lengo la kuwatapeli na kujipatia fedha isivyo halali.

Operesheni hiyo iliyoafanyika nchi nzima  imefanikiwa kukamata watu kadhaa wanaojifanya ni Maafisa wa NIDA na wanaochapisha Nakala Tepe (Online Copy) wakiwemo wafanyabiashara wa maduka ya Steshenari. 

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geofrey Tengeneza amesema Alhamis Tarehe 14/09/2023 wamefanikiwa kumkamata mtu mwingine anayefahamika kwa jina la Gibson Buberwa aliyejifanya ni Mratibu wa NIDA kutoka Ilala, Dar es Salaam.

 

Mtu huyo alikamatwa na maafisa wa NIDA kwa kushirikiana na jeshi la polisi mtaa wa Majengo, Kata ya Vingunguti akiwa na fomu za Usajili wa watu zinazotumiwa na NIDA baada ya kuwekewa mtego na hatimaye kunaswa.

Amesema mtu huyo alikuwa akitumia fomu hizo za NIDA kuwasajili watu akiwaaminisha kuwa watapata Vitambulisho vya Taifa na kuwataka kutoa malipo ya shilingi 5,000 kwa kila mtu. Ametoa onyo kwa watu ambao si watumishi wa NIDA kuacha mara moja kujifanya ni maafisa wa NIDA na kutapeli wananchi. 

Kuhusu huduma ya Online Copy Tengeneza amesema NIDA ilikwisha sitisha huduma ya Nakala Tepe (Online Copy) toka mwaka 2019 na kwamba yeyote anyetangaza kutoa huduma hiyo ni mhalifu na akifahamika atachukuliwa hatuka kali za kisheria. Amewataka wananchi kuendelea kutumia Namba zao Utambulisho hadi pale watakapopata vitambulisho.

“Tunashukuru kwa ushirikiano tunaupata kutoka Maafisa wa Serikali za Kijiji/Mtaa pia tunatoa wito kwa mtu mwenye taarifa juu ya matapeli aweze kufahamisha Jeshi la Polisi au awasilishe kwenye Ofisi za NIDA za Wilaya.” alisema na kuongeza kuwa watu wote wanaotumia jina la taasisi kufanya utapeli wanatakiwa kuacha mara moja, kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria na wakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria,

About the author

mzalendoeditor